Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAWAKE 5 GGML WAHITIMU MAFUNZO YA UONGOZI, GWAJIMA AWAFUNDA


Mmoja wa wahitimu wa programu ya mafunzo ya uongozi (FFT) kwa mwama huu, Kulwa Nyirenda anayefanya kazi GGML, akipokea cheti kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima (wa tatu kushoto) , wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira & Watu Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, nao kutoka kulia kwenda kushoto: Makamu Mwenyekiti wa ATE, Imelda Lutebinga, Mwenyekiti Mstaafu wa ATE, Almas Maige na Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Mafunzo ya Utawala Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), Profesa Lucky Yona.
Mmoja wa wahitimu wa programu ya mafunzo ya uongozi (FFT) kwa mwama huu, Zuhura Khamis anayefanya kazi GGML, akipokea cheti kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima (wa tatu kushoto) , wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira & Watu Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, nao kutoka kulia kwenda kushoto: Makamu Mwenyekiti wa ATE, Imelda Lutebinga, Mwenyekiti Mstaafu wa ATE, Almas Maige na Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Mafunzo ya Utawala Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), Profesa Lucky Yona.
Makamu Rais wa AngloGold Ashanti - GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu hao.
JUMLA ya wafanyakazi watano wanawake kutoka Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) wamehitimu mafunzo ya juu ya uongozi na kutakiwa kutumia elimu waliyoipata kwenda kubadilisha kampuni wanazofanyia kazi na jamii zao.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambayo ni ya tisa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, hutolewa kwa wanawake ili kuwawezesha kuwa na ujuzi na uwezo wa kushika nafasi za juu za uongozi kwenye kampuni zao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mahafali ya tisa ya mafunzo hayo yaliyojumuisha wahitimu 76, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amezipongeza kampuni zilizowafadhili wafanyakazi wao wanawake kwa kushiriki mafunzo hayo.

Pia alisema Serikali itaendelea kuunga mkono programu zinazotekelezwa na ATE hasa ikizingatiwa zinalandana na mipango ya serikali katika kuimairisha na kuhamasisha usawa wa kijinsia.

Alisema kaulimbiu ya mahafali hayo yaliyoambatana na mkutano mkuu wa sita wa ATE, inayosema ‘Wekeza kwa mwanamke kuongeza kasi ya maendeleo’ imekuja wakati muafaka ambao wizara yake inakwenda kuzindua sera ya taifa ya jinsia na maendeleo.

Alisema sera hiyo itazinduliwa rasmi tarehe 8 Machi mwaka huu ikiwa ni katika kilele cha sherehe za kimataifa za siku ya mwanamke.

"Nitoe rai kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kuendelea kutoa mafunzo haya ya uongozi kwa wanawake pamoja na kuendelea kuwa vinara katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa maeneo ya kazi. Vilevile, hakikisheni mnahimiza waajiri na wanawake viongozi kuzingatia kuweka mifumo na mazingira rafiki ya kupiga vita ukatili wa kijinsia kwenye maeneo ya kazi, kwani matukio hayo yapo na kuna baadhi ya maeneo ya kazi hayasikiki kwa kuwa hakuna mazingira rafiki" amesisitiza Dk. Gwajima.

Akichangia mjadala katika hafla hiyo, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti - GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo alisema tangu mafunzo hayo yaanzishwe tayari GGML imewezesha wafanyakazi wanawake 23 kupata elimu hiyo.

Amesema baadhi yao wamepandishwa vyeo huku wawili wakipata nafasi za juu za uongozi ndani ya kampuni hiyo.

Alisema mafunzo hayo yamekuwa chachu kwa kampuni hiyo kwani yameongeza ushirikiano mkubwa kati ya wafanyakazi na kuimarisha usawa wa kijinsia.

Amesema baadhi yao pia wamekuwa na uwezo wa kushindana kimataifa katika nafasi zao ikiwamo wahandisi wanawake.

“GGML imeendelea kuunga mkono mafunzo haya kuimarisha usawa wa kijinsia lakini pia suala hili limeendelea kutekelezwa ipasavyo na wafanyakazi wenyewe kutoka ndani ya mioyo yao,” alisema Shayo.

Mmoja wa wahitimu hao wa GGML, kutoka Idara ya Fedha, Tammy Sumawe aliushukuru uongozi wa kampuni hiyo kwa kuwahamasisha wanawake kushiriki mafunzo hayo ambayo yamekuwa chachu kwao na hata kwa maisha yap kutokana na mambo wanayofundishwa.

Naye Profesa Lucky Yona ambaye ni mmoja wa wakufunzi hao kutoka Chuo cha Mafunzo ya Utawala Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), alisema wanafunzi hao wamefundishwa namna ya kuongoza, kuzungumza katika mikutano na vikao vya hadhi ya juu pamoja na mafunzo mengine yanayowezesha wahitimu kuwa na sifa za uongozi.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran alisema zaidi ya wanafunzi 400 tayari wamehitimu mafunzo hayo kutoka makampuni mbalimbali nchini.

"Nawapongeza wahitimu wa mafunzo ya Programu ya Mwanamke Kiongozi Awamu ya 9, niwaombe wakaweke juhudi na tija na kuishi mafunzo waliyopatiwa na kutumia nafasi zao za uongozi kuleta mafanikio katika sehemu zao za kazi lakini zaidi kwa jamii inayowazunguka," alisema Suzanne.

Wahitimu wafahyakazi wanawake kutoka GGML waliohitimu mafunzo hayo ni pamoja na Cecilia Nkanabo, Kulwa Nyirenda, Njile Izengo, Zuhura Khamis na Tammy Sumawe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com