Shirika la Grumeti Fund limetoa ng'ombe wa maziwa 15 wenye thamani ya Mil. 52 kwa vijiji vya Motukeri na Nyichoka wilayani Serengeti na vijiji vya Mugeta na Tingirima wilayani Bunda,ikiwa ni awamu ya kwanza ya mradi huo unaolenga kuhamasisha ufugaji wenye tija na unao tunza mazingira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumeti Fund Bi. Frida Mollel amesema lengo la mradi huo ni kuondoa changamoto za kimazingira na mabadiliko ya tabia ya tabia nchi sambamba na kuhamasisha ufugaji wenye faida na kuongeza kipato na lishe Bora katika kaya.
"Mradi huu uliobuniwa na Grumeti Fund unalenga kupunguza changamoto za kimazingira kwakuwa na ufugaji wenye tija kwa kutumia nafasi ndogo lakini matunda yake ni makubwa na wanufaika wa mradi huu wapo 15 ambao 8 ni kutoka vijiji vya Serengeti na wananchi 7 wakitoka katika vijiji vya Wilaya ya Bunda" alisema Bi. Frida
Aidha Bi. Frida amesisitiza utunzaji wa ng'ombe hao sambamba na kuzingatia taratibu za mradi ili kuufanya kuwa endelevu na wenye manufaa kwa wananchi wengi.
Vilevile, ameongeza kuwa Ng'ombe wote 15 wanamimba na wamepatiwa chanjo muhimu, ambapo pia Grumeti Fund imetoa mbegu za majani ya malisho kwa wanufaika wote ili kuhakikisha upatikanaji wa malisho kwa mwaka mzima.
Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji amewataka wananchi kuzingatia taratibu zote za mradi na kuwataka kuutumia mradi huo kama darasa la mabadiliko kuachana na ufugaji holela na kuingia katika ufugaji wa kisasa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Anney amewataka wanufaika wa mradi huo kuutumia vizuri ili kujikwamua katika umasikini kwa kupitia mazao yatakoyopatikana katika ng'ombe hao huku akiwataka wanufaika wa mwanzo kuwa chachu ya ushawishi kwa taasisi ya Grumeti Fund kuleta Mradi wa awamu ya pili.
Sambamba na hayo, baadhi ya wanufaika wa mradi huo wameeleza shukrani zao kwa Kampuni ya Grumeti Fund huku wakiutaja Mradi huo kama chanzo cha kukata mnyororo wa umasikini katika familia zao na kuahidi kuwatunza ng'ombe hao ili kuongeza idadi ya wanufaika.
Grumeti Fund katika awamu ya kwanza ya Mradi imetoa ng'ombe kwa Wananchi 15 huku katika awamu ya pili wakitarajia kutoa ng'ombe 15, awamu ambayo itategemea mafanikio yatakayopatikana katika awamu ya Kwanza.
Social Plugin