Katibu Mtendaji Baraza la Sensa ya Filamu na Utamduni Dkt. Omar Abdalla Adam akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na kuzuia shughuli zote za sanaa na burudani katika kipindi cha maombolezo kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Mhe. Ali Hassan Mwinyi,hafla iliyofanyika ofisi za BASFU Mwanakwerekwe Zanzibar.
Na Rahma Khamis Maelezo
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imepiga marufuku upigaji wa muziki wa aina yoyote katika kumbi za starehe na burudani nchini.
Tamko hilo limetoa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Sensa ya Filamu Dkt. Omar Abdalla Adam huko Ofisini kwake Mwanakwerekwe wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kifo cha Rais Mstaafu Al-hajj Ali Hassan Mwinyi kilichotokea jana.
Amesema hatua hiyo imekuja mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Drkt Samia Suluhu Hassan kutangaza kifo cha mstaafu huyo na kutoa siku 7 za maombelezo kuanzi leo.
Amesema kwa mujibu wa kifungu 8(1),(d) cha sheria nambari 7 ya 2015 ya Baraza la Sanaa , Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar, Baraza limepiga marufuku shughuli zote za Sanaa na burudani katika maeneo ya starehe na burudani Zanzibar yakiwemo maeneo ya kijamii,hoteli, kumbi na Baa.
Katibu huyo amewaomba wananchi kushirikiana katika kipindi hiki cha msiba kufuata agizo hilo kwa kutopiga ngoma katika shuguli zao zote ikiwemo dufu na miziki mengine isipokuwa utaratibu wa akdi utaendelea kufanyika kama kawaida bila ya sherehe yoyote
“Harusi kama utamaduni wetu ziendelee kufanyika kama kawaida katika familia zetu isipokuwa hakutakuwa na upigaji wa ngoma na sherehe nyengine kutokana na utamuduni mila na silka zetu,”alifafanua Dkt Omar.
Ameeleza kuwa tukio hilo ni la kitaifa hivyo atakaekwenda kinyume na tamko hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufungwa kwa muda miezi sita( 6) ama kulipa faini ya sh million 1.
Aidha amefahamisha kuwa kuanzia leo baraza litafanya doria katika kumbi na sehemu zote za starehe ili kuwabaini watakaokwenda kinyume na agizo hilo na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hata hivyo Katibu Mtendaji amewashauri wale ambao wameshaweka oda kwa ajili ya shughuli katika kipindi hiki kuwarejeshea fedha zao ama kufanya mazungumzo baina yao ili kupisha siku za maombolezi na baadae kuendelea na shughuli hizo .
Marehemu Al-hajj Mwinyi alifariki dunia febuari 29,2024, katika Hospitali ya Mzena Dar-essalam na kutarajiwa kuzikwa machi 02 mwaka huu kijijini kwao Mangapwani Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.