Na John I. Bera
Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu zimepanga kushirikiana kimkakati ili kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zinazopatika kwenye sekta ya Maliasili na Utalii.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 9, 2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb) alipotembelea Banda la Maliasili na Utalii kwenye Maonesho ya Wiki ya Wanawake Duniani yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma
Mhe. Gwajima amesema Wizara yake ni Wizara mtambuka ambayo utendaji kazi wake unategemea Wizara zingine ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii
"Natambua kuwa ninyi ni wadau wetu muhimu kwa sababu sisi Wizara ya Maendeleo ya Jamii hatuwezi kuendelea pekee yetu pasipo sekta nyingine ikiwemo sekta ya Maliasili na Utalii", amesema Mhe. Gwajima.
Mhe. Gwajima amesisitiza kuwa ili kuwafikia wanawake katika maeneo mbalimbali nchini wizara za kisekta haziwezi kuachwa pembeni ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii.
Aidha, Waziri Gwajima ameipongeza Wizara ya Maliasili kwa kushiriki kwenye Maonesho hayo huku akisisitiza kuwa anaamini ya kuwa Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara yake kuhakikisha kuwa Wanawake wanajihusisha na shughuli za utalii nchini.
Akizungumza mbele ya Waziri Gwajima, Afisa Wanyamapori Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Africo Mattogoro amesema wao kama Wanawake kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wanayo ari ya kufanya kazi ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa Rasilimali za Wanyamapori na maeneo oevu kwa ajili ya kuunga mkono agenda ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu yake ya “The Tanzania Royal Tour’’
Ameongeza kuwa wao kama Wanawake ambao ni Wahifadfhi kutoka Wizara hiyo wanaendelea na jitihada mbalimbali za kuelimisha jamii kuhusu suala zima la uhifadhi hususani kwa wakinamama ambao wamekuwa wakiingia kwenye maeneo ya Hifadhi na kuendesha shughuli za kibinadamu bila kujua ya kuwa wanaharibu mazingira na uhifadhi kwa ujumla
Amesema Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake imekuwa ikitumia njia mbalimbali za kuwezesha Wanawake ikiwemo kutumia Vikundi mbalimbali kama COCOBA na njia nyinginezo kwa lengo la kuinua uchumi wa wanawake wa Kitanzania. Jitihada hizo zinafanikiwa kwa kupitia taasisi za uhifadhi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama vile TANAPA, TAWA, TFS, NCAA na kwa kushirikiana na wadau wa mbalimbali wa Uhifadhi kwa kuwawezesha wananchi kupitia vikundi kwa kuanzisha na kuwawezwsha shughuli mbadala rafiki na mazingira mfano ufugaji nyuki.
Social Plugin