Watu 9 wamekufa maji baada ya gari yao iliyokuwa ikitokea kijiji cha Tingi kuelekea Kijiji cha Nyoni kusombwa na maji eneo la kijiji cha Lumeme Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco Chillya amesema atu hao walikuwa wakisafiri na gari aina ya Noah Toyota lenye namba za usajili Na T. 770 DBU mbayo ni mali ya John Agaton Kapinga mkazi wa Kijiji cha Lumecha lilisombwa na maji baada ya dereva wake kufanya uamuzi wa kizembe kulazimisha kuvuka daraja la chini likiwa limejaa maji yaendayo kasi.
Kamanda SACP Chillya, amesema, dereva huyo ametambulika kwa jina la Edwin Abel Ngowoko (55), pamoja na abiria wake nane walikufa baada ya gari kusombwa na kugeuza uelekeo kufuata mto na kukwama kwenye korongo ndani ya Mto Kisima Kitongoji cha Lumeme Mpepo Wilayani Nyasa.
Amesema tukio hilo lilitokea Tarehe 11/3/2024 Saa 12:30 jioni ambapo abiria na Dereva wao walishindwa kujiokoa baada ya nguvu ya maji kuwashinda na milango kushindwa kufunguka na wote walipoteza maisha.
Kamanda SACP Chillya amewataja waliofariki na umri wao kuwa, Dereva Edwin Abel Ngowoko (55) Mkazi wa kijiji cha Mbanga, Valeriana Ndunguru (18) Mkazi wa Kijiji cha Mbanga, Innocent Kasian (63) Kijiji cha Mbanga, Saimon Mahai (21) Mkazi wa kijiji cha Kingerikiti.
Wengine ni Nathan Kumbulu (39) wa kijiji cha Mbanga, Faraja Daudi Tegete(18) ambaye ni mwanafunzi Kidato cha Tatu Shule ya Sekondari Kilumba Kata ya Lumeme Nyasa. Pia amemtaja mtoto Mwenye umri wa miaka 2 Ebiati Daudi Tegete Mkazi wa Kijiji cha Lumeme.
Wengine ni Alfonsia Kasian Mbele (40) Mkazi wa Kijiji cha Lumecha na Solana Thomas Ndunguru (16) Mkazi wa Mbanga.
Kamanda SACP Chillya amesema miili ya marehemu wote imeopolewa na kuhifadhiwa katika Zahanati ya Lumeme wilayani Nyasa kusubiri Uchunguzi wa Daktari na baadae kuwakabidhi Ndugu kwa mipango ya mazishi.
Kamanda SACP Chillya ametoa onyo kwa madereva wote wa vyombo vya moto kuacha kabisa kuyakadiria au wasipime maji kwa macho ni hatari kwa usalama wa maisha ya watu na vyombo na mali zao.
Social Plugin