TABATA MTAMBANI WAKATAA ONGEZEKO HOLELA ADA YA UZOEAJI TAKA


Na Editha Majura _  Dar es salaam

WANANCHI wa Tabata, Mtaa wa Mtambani, Jijini Dar es Salaam wamekataa ongezeko la ada ya uzoaji taka, kutoka Sh 2,500 hadi Sh 5,000  kinyume na Sheria ndogo za (Afya na Usimamizi wa Mazingira) za Halmashauri ya Manispaa ya Ilala za Mwaka 2019.

Jedwali la Kwanza lililotungwa chini ya kifungu cha 5(1) inaelekeza; Na 2: Nyumba za chini (kwa kaya) kipato cha juu kwa mwezi ni Sh 8,000, kipato cha kati Sh 3,500 na kipato cha chini ni Sh 2,500.

Lakini Kampuni ya BP Urasa, inayotoa huduma hiyo kwenye Mtaa huo inatumia mkusanya ada hizo, Rebeka  Shaban kufikishia wakazi hao andiko linalowataka kulipa 5,000 kuanzia  Machi 01 Mwaka huu.

Hivi karibuni, kwenye mkutano wa hadhara, mmoja wa wakazi hao alihoji uhalali wa andiko hilo lenye nembo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Halmashauri ya Ilala, muhuri wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Tabata na saini ya Afisa Afya wa Kata hiyo.


Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Brigitte Nchimbi akasema; “Hili andiko silitambui, ni feki, tunalipa Sh 2,500  hakuna kikao kilichoamua tulipe Sh 3,000 au Sh 5,000, lipeni 2,5000 na wawape risiti.”


Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, George Lugongo, amesema anaandaa mkutano wa hadhara ambao pamoja na mengine, suala hilo litajadiliwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post