Na Mariam Kagenda _ Kagera
Wadau wa group la Whatsapp lijulikanalo kama Bukoba Mjini mpya kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Stephen Byabato wametoa msaada wa saruji mifuko 20 kwa ajili ya ujenzi wa msikiti pamoja na mitungi 15 ya gesi kwa mama lishe katika kisiwa cha Musira kilichopo kata ya Miembeni Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Wakati akipokea misaada hiyo Diwani wa kata ya Miembeni Richard Gaspar kwa niaba ya wananchi wa kisiwa cha Musira amewashukuru wadau wa group hilo pamoja na mbunge wa Jimbo la Bukoba kwa kuikumbuka jamii ya Musira kwani Saruji hiyo itasaidia katika ujenzi wa Msikiti wa waumini wa dini ya kiislamu kwenye kisiwa hicho na mitungi ya gesi itawasaidia mama lishe kurahisisha shughuli zao kwani walikuwa wanapata shida kupata mkaa hasa kipindi cha mvua.
Naye mmoja wa wanakamati walioratibu shughuli ya misaada hiyo kutoka Group la Whatsapp la Bukoba Mjini Mpya, Jamila Emily amesema kuwa ikiwa ni mwendelezo wa group hilo kuigusa jamii ya wana Bukoba mjini waliona katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani waguse kwa wananchi wa kisiwa cha Musira kwa kutoa Saruji ya kuwezesha ujenzi wa msikiti ili wananchi wa kisiwa cha Musira waweze kuswalia sehemu salama .
Emily amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Stephen byabato pamoja na wadau wa maendeleo kutoka group la Bukoba mjini mpya na wanakamati walioratibu swala hilo kwa kuona umuhimu wa jambo hilo na kutoa michango ya kufanikisha kupatikana misaada iliyotolewa.
Naye mwenyekiti wa Msikiti wa Musira Yakub Fresh amesema kuwa msaada huo utasaidia kutatua changamoto iliyopo kwani kwa sasa wanaswalia katika kibanda cha mtu sehemu ambayo sio salama ambapo baada ya uwepo wa changamoto hiyo waliamua kuanzisha ujenzi wa msikiti ambao umefikia hatua ya madirisha hivyo Saruji hiyo itasaidia kupiga hatua kubwa ya ujenzi wa Msikiti ili waweze kupata msikiti wa kuswalia
Nao Mama lishe waliopokea majiko ya gesi wamesema kuwa sasa kisiwa cha Musira kinaenda kuwa kisiwa cha mfano kwa utumiaji wa nishati salama .wameshukuru kuletewa msaada wa gesi na kusema kuwa wateja wao watakuwa wakipata chakula cha moto wakati wote kwani hapo awali walikuwa wanapata changamoto ya mkaa kuutoa nchi kavu kuuleta katika kisiwa hicho wakati mwingine ulikuwa unafika ukiwa umeshalowa na maji hivyo kwa sasa hawatoangaika tena na mkaa jambo ambalo litasaidia wateja wao kupata huduma nzuri ya chakula wakati wote.
Wanakamati walioratibu msaada wa Musira