Na Ferdinand Shayo ,Dar es Salaam.
Kituo cha zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kimepatiwa mashine maalumu ya kumenya ganda laini la korosho na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) kwa lengo la kusaidia kiwanda darasa kilichoanzishwa wilayani Manyoni Mkoani Singida.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa mashine hiyo Jijini Dar es salaam inayojulikana kitaalamu kama peeling machine,Kaimu Mkurugenzi wa Camartec Mhandisi Pythias Ntella ameishukuru TIRDO kwa kuwapa mashine hiyo itakayosaidia kuongeza kasi ya ubanguaji wa korosho katika kiwanda darasa cha kubangua korosho kilichopo Wilayani Manyoni Mkoani Singida.
Ntella amesema kuwa mashine hiyo itawawezesha kuongeza kasi ya ubanguaji wa korosho ili kufikia adhma ya serikali ya kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zinazozalishwa zinabangulia nchini ifikapo mwaka 2025/26 hivyo kupunguza uuzaji wa korosho ghafi katika masoko ya nje ya nchi.
"Tunawashukuru sana TIRDO kwa kutoa mashine hii ili kuunga mkono ndoto ya kiwanda hiki na viwanda Vingine vya kubangua korosho ambavyo vitakua mkombozi kwa wakulima" anaeleza Ntella.
Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) Prof. Mkumbukwa Mtambo amempongeza Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutosha kuwezeshwa utengenezaji wa mashine mbali mbali ikiwemo mashine waliyoitoa kwa CAMARTEC ya kumenya ganda laini la korosho.
Prof. Mtambo amesema kuwa ushirikiano ulioko kati ya TIRDO na CAMARTEC ni mkubwa katika Kuhakikisha wanaanzisha viwanda darasa vya kubangua korosho na kuwasaidi wakulima wa kitanzania kuongeza thamani ya mazao na kupata bei nzuri katika soko.