Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UJENZI BANDARI YA MWANZA KASKAZINI


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa ujenzi, upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini iliyopo Jijini Mwanza.

Hayo yamesemwa tarehe 16 Machi, 2024 Jijini Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Seleman Kakoso ( Mb) wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi, upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini.

“ Kamati inaridhika na usimamizi wa mradi huu pamoja na miradi mingine yote ya TPA ambayo imetembelewa. Simamieni huu mradi uweze kukamilika kwa wakati na kuwa na tija kwa Watanzania”, amesema Mhe. Kakoso.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile ( Mb) akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, amesema Wizara imepokea maoni, mapendekezo na maelekezo ya Kamati na itaenda kuyafanyia kazi na kuyatekeleza.

Mradi wa Utekelezaji wa ujenzi, upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 18.6 na utachukua miezi 18 kukamilika kwake ambapo hadi sasa umefikia Asilimia 30%.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com