Na Mwandishi Maalum
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) kumsimamia mkandarasi kampuni ya CHICO anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Noranga-Itigi (km 25) na Doroto - Noranga (km 6) kwa kiwango cha lami kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.
“Wizara hakikisheni Wmnamsimamia Mkandarasi huyu akamilisha kipande cha barabara alichopewa kukijenga kwa wakati, huko wananchi wanasubiri mradi huu kwa hamu ambao utachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii", amesema Kakoso.
Aidha, Kamati imesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo Wakandarasi wa ndani kwa kuwapa ujenzi wa miradi ya barabara yenye urefu wa kilometa 50 hadi 100 na kuwaunganisha na Kitengo cha Usimamizi wa miradi kutoka TANROADS (TECU) ili kupata ujuzi na kuboresha taaluma ya uhandisi nchini.
“Wizara endeleeni kulisimamia hili la kuwaandaa watanzania walio wengi katika miradi ya Serikali kwani faida zipo nyingi kwa makampuni yetu, ajira kwa wananchi na kwa Taifa letu kiujumla”, amesisitiza Kakoso
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiahidi Kamati kuwa Wizara itaendelea kusimamia kwa ukamilifu suala la ushirikishwaji wa Wakandarasi wazawa katika miradi ya barabara sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ili kuweza kupata maarifa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi nchini.
Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Doroth Mtenga ameeleza kuwa mradi huo wa barabara ya Noranga - Itigi (Km 25) unagharimu shilingi Bilioni 29.7 ambapo umefikia asilimia 74.4 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2024.
Eng. Mtenga ameeleza kuwa mradi huo umetoa ajira 274 kati ya hizo ajira 256 zimetolewa kwa Watanzania sawa na asilimia 93.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Eng. Msama Msama ameieleza Kamati kuwa Serikali imelipa fidia kwa wananchi 656 ili kupisha ujenzi wa mradi huo ambapo jumla ya Shilingi Milioni 721.974 zimetumika.
Social Plugin