Na Mariam Kagenda -Kagera
Mbunge wa Jimbo la Ngara mkoani Kagera Mhe. Ndaisaba Ruholo amesema katika kipindi cha miaka 3 wilaya hiyo imeweza kupata miradi mikubwa ya maendeleo tofauti na kipindi cha nyuma jambo ambalo linatakiwa kuwafanya wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuwa na imani na serikali yao.
Mhe. Ndaisaba Ruholo ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ngara amesema hayo wakati wa mikutano yake ya adhara ya kuzungumza na wananchi kuwaeleza yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 3.
Amesema kuwa ahadi nyingi alizozitoa wakati akiomba ridhaa kwa wananchi hao hasa katika sekta ya elimu, afya, maji pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara ambazo zilikuwa hazipitiki na bado kuna miradi mikubwa ya maji na barabara inayoendelea kutekelezwa.
Amesema kuwa katika miradi inayoendelea kutekelezwa na iliyopo katika hatua za kuanza kwa ujenzi ni pamoja na ujenzi wa soko, serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa soko la kimkakati la Kabanga jambo ambalo lilikuwa ni moja kati ya ahadi alizowaahidi wananchi wa wilaya hiyo kumpa ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Kabanga ,Hafidh Abdalla amesema kuwa mwaka 2020 waliahidi kuwatetea wananchi lakini kumekuwa na tatizo la migogoro ya ardhi bado ni changamoto kwani wananchi wanategemea kilimo na ufugaji hivyo watahakikisha wanawatetea wananchi kuhusiana na suala hilo.
Social Plugin