Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Kamati ya kudumu ya bunge ya miundombinu imetembelea ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano uliopo manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga.
Ziara hiyo ya ukaguzi imefanyika leo Machi 14, 2024 katika ofisi za Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL mkoani humo.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa mkondo wa taifa wa mawasiliano mbele ya kamati ya kudumu ya bunge Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Peter Ulanga amesema ujenzi wa mitambo ya kuongeza uwezo kituo cha mkongo Shinyanga umekamilika kwa 100% na mitambo inafanya kazi ambapo ujenzi huo umegharimu zaidi ya kiasi cha bilioni 1 huku akieleza changamoto katika utekelezaji wa mitambo hiyo.
"Awamu ya kwanza ya ujenzi wa mkongo wa taifa ilianza 2009 ikiwa na uwezo wa 40G na baadae kuongeza uwezo kwa 200G hadi 400G kwa Singida - Shinyanga - Mwanza, ujenzi wa faiba kutoka Shinyanga mpaka Kahama umekamilika kwa 100% ambao umegharimu kiasi cha milioni 594", amesema Peter Ulanga.
"Zipo changamoto ambazo tulikumbana nazo katika utekelezaji wa ujenzi huu ni pamoja na kupata tatizo la umeme, imekuwa ni changamoto TANESCO kuzima umeme kwa wakati ili kupisha ujenzi huu ambapo imepelekea kuchelewa kukamilika kwa mradi, hali ya hewa ya mvua ni moja ya changamoto ya mazingira ya kufanyia kazi katika usimikaji nguzo na kuvuta waya", ameongeza
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Nnauye ameeleza ushirikiano uliopo kati ya TTCL na TANESCO katika usambazaji wa mkongo wa taifa kwenye maeneo mbalimbali.
"Katika kupanua mtandao wa mkongo huu hadi kwenye mipaka ya nchi yetu tumeendelea kusambaza kwenye nchi jirani ikiwemo Kenya, Uganda na Rwanda na sasa tunataka kuingiza mkongo huu nchini Congo ambapo mpaka sasa taratibu kadhaa zimekwisha chukuliwa, nikuhakikishie Mwenyekiti kuwa tunatambua kuwa tuna dhamana kubwa ya kuhakikisha tunaziunganisha nchi za pembezoni", amesema Nnape.
Mwenyekiti wa kamati Selemani Kakoso, ambaye ni mbunge wa jimbo la Mpanda vijijini ameipongeza wizara hiyo kwa jitihada mbalimbali inazofanya kuhakikisha uwepo wa uhakika wa mawasiliano sehemu zote na kuitaka TTCL kujiendesha kibiashara.
"Kamati inampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu tunaona jitihada inayofanywa na wizara yake kwa kufanya mapinduzi makubwa ya mawasiliano kwa kipindi kifupi, tunachoomba msimamie kikamilifu mkongo wa taifa ujisimamie kibiashara kwa sababu mnatoa huduma zinaleta fedha nyingi kwa kufanya ubunifu na usimamizi mzuri, suala la mkataba wa TTCL na TANESCO naomba Mheshimiwa Waziri mkapitie upya mkataba huu muangalie maeneo ambayo yatakuwa na afya ili TTCL iweze kujisimamia", amesema Kakoso.
Mtambo wa usambazaji mkongo wa taifa uliopo mkoani Shinyanga.
Kamati ya bunge ikikagua mtambo huo.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mbunge wa Jimbo la Mtama Mkoani Lindi Mheshimiwa Nape Moses Nnauye akizungumza wakati wa kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Jengo la ofisi ya TTCL Mkoa wa Shinyanga.
Picha ya pamoja.
Social Plugin