Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAPE ATEMBELEA KIWANDA CHA VIFAA VYA KIELEKTRONIKI ARUSHA

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), alitembelea kiwanda cha TANZTECH jijini Arusha na kupokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw. Gurveer Hans.

Mhe. Nape amefanya ziara hiyo leo tarehe 19 Machi, 2024 na kujionea kiwanda cha kuunganisha vifaa vya kielektroniki kama simu janja, vishikwambi, kompyuta, na vifaa vingine vya kielektroniki.

Katika ziara yake, Waziri Nape amepongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa uwekezaji mkubwa waliofanya katika sekta ya mawasiliano ya simu. 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Bw. Gurveer Hans amesema kiwanda cha TANZTECH ni kiwanda cha kwanza nchini Tanzania kinachoendeshwa kwa ushirikiano na wachina ambao pia wamewekeza kwenye kiwanda kama hiki katika nchi za Uganda na Ethiopia.

Akielezea kuhusu kiwanda hicho, Bw. Hans amesema hivi sasa kiwanda hicho kimeanza kuunganisha simu janja 40,000 kwa mwezi, vishkwambi 30,000 kwa mwezi, laptop 15,000 na projector 10,000 kwa mwezi.

Bw. Hans ameiomba serikali kuondoa kodi ya mapato kwenye vifaa vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi na wakati wa kuuza vifaa hivyo vya kielektroniki ili kupunguza gharama za uzalishaji.

Waziri Nape amewapongeza kwa uwekezaji huo na kupokea maombi yaliyowasilishwa na uongozi wa kiwanda na kuahidi kuyafanyia kazi. Ameupongeza pia uongozi wa kiwanda cha TANZTECH kwa kuajiri wafanyakazi wazawa ambapo asilimia 90 ya wafanyakazi hao ni wanawake.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com