Na Christina Cosmas, Morogoro
MBUNGE wa jimbo la Kilosa mkoani Morogoro Prof. Paramagamba Kabudi amewahimiza wazazi katika kijiji cha Kitange mbili kata ya Mtumbatu kuweka utaratibu wa kuwaruhusu watoto kwenda shule kwa manufaa yao na kuacha tabia ya kuwazuia na kusababisha kuwepo kwa idadi ndogo ya watoto walioripoti kuanza kidato cha kwanza katika shule ya sekondari kitange.
Prof. kabudi ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua miradi ya shule ambapo amefika katika shule hiyo ambayo ujenzi wa vyumba vya madarasa unaendelea huku akiwataka wananchi hao kuhakikisha watoto wanakwenda shule ili kuunga mkono juhudi za serikali inayotoa fedha kwaajili ya ujenzi wa shule.
Shule hiyo mpya ya sekondari Kitange ujenzi wake ulianza mwaka 2022 kwa nguvu kazi ya wananchi baada ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wa takribani zaidi ya kilometa 10 kufuata huduma ya shule ambapo hadi sasa ni madarasa mawili pekee ndio yaliyokamilika kwa hatua ya awali kwaajili ya wanafunzi kuanza masomo kwa kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa 2024.
Akitoa taarifa ya mradi huo mkuu wa shule hiyo Cecilia Chipeta amesema Licha ya wananchi kuanza kwa kujitolea nguvu kazi wadau na serikali haikuwaacha nyuma na sasa ujenzi wa vyumba vingine vya madarasa unaendelea huku akibainisha kuwa wanafunzi 84 pekee ndio walioripoti shule kati ya wanafunzi 198 wa kidato cha kwanza waliopangiwa katika shule hiyo.
Selina shayo ni katibu wa wazazi cha chama cha mapinduzi(CCM) wilaya ya kilosa anasikitishwa na taarifa hiyo ya watoto kutohudhuria shule na kuwahimiza wazazi kuona umuhimu wa elimu kwa watoto ikiwa ni Pamoja na kuwasaidia kujimudu katika maisha yao ya baadae.
Naye Diwani wa kata ya Mtumbatu Amani Sewando aliahidi kushirikiana na viongozi wa kijiji hicho kutafuta wanafunzi ambao bado hawajaripoti shule na kuhakikisha wanaripoti shuleni.
Licha ya kutembelea shule hiyo ya sekondari kitange mbunge Prof. Kabudi amefanikiwa kukagua ujenzi wa shule ya sekondari Dumila ambayo ujenzi wake unagharimu takribani kiasi cha shilingi milioni 125 huku hadi sasa ambapo kiasi cha zaidi ya milioni 123 kikiwa kimeshatumika.
Social Plugin