Katika kipindi cha Miaka Mitatu cha Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan madarakani, Serikali ya awamu ya sita imefanya mageuzi makubwa ya Miundombinu ya Ujenzi wa Barabara na madaraja Mkoani Katavi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala ya Barabara ( TANROADS) Mkoa wa Katavi Mha. Martin Mwakabende, alipozungumza na waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.
Amesema “ Tunampongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Mpanda-Tabora (km 337.429),sehemu ya pili ni Komanga-Kasinde ( Km 108), pamoja na Barabara ya Kasinde-Mpanda (Km 105.389) ndani ya miaka mitatu.”.
Amesema, miradi mingine ya kimkakati na ya kitaifa inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na Barabara ya Mpanda-Uvinza-Kanyani (km 250.44), Kibaoni- Sitalike, sehemu ya Kibaoni-makutano ya mlele (km50), Barabara ya Kagwira-Karema (km 110.29), ujenzi wa kitanda cha Daraja la Kavuu ( urefu wa mita 87.5)
Vilevile, Ujenzi wa Daraja jipya la Mirumba (mita 60), Daraja jipya la Mto Lugufu ( mita 42) ambalo kukamilika kwa Daraja hilo kutatatua changamoto ya muda mrefu ya wakazi wa Mishamo na Lukoma.
“ Miradi hii itakapokamilika itasaidia sana Wananchi wa katavi kwani itarahisisha usafiri na usafirishaji wa kutoka Katavi kwenda Kigoma, Mbeya na mikoa mingine kwa haraka zaidi kwani Serikali inaenda kufungua Mkoa wa katavi kwa miundombinu ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.” Ameeleza Mha. Mwakabende.
Amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa kufunga Jumla ya taa 719 sawa na asilimia 77.15 , na kufanya Mkoa wa Katavi Uwe na Jumla ya taa 932 zenye thamani ya Shilingi bilioni 2.
Pia, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kulinda Miundombinu ya barabara pamoja na hifadhi ya barabara kwani kufanya hivyo kutapelekea barabara zidumu kwa muda mrefu zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Miradi ya Maendeleo kutoka TANROADS Katavi, Mha. Albert Laiza amesema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwaletea fedha za kufanya Matengenezo ya barabara.
Naye Mkandarasi mzawa anayetekeleza ujenzi wa Daraja la Kavuu lenye urefu wa mita 87.5, Mha. Bernad Ngailo kutoka Kampuni ya Ngetijo Group Co. Ltd amesema katika kipindi hiki cha Miaka mitatu Serikali imeweza kuwajali na kuwaamini wakandarasi wa ndani kwa kupewa kujenga miradi mikubwa ya kimkakati.
Social Plugin