REA YATUMIA TRILIONI 1.102 KUPELEKA HUDUMA KWA WANANCHI PWANI

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge la Nishati Dk. Mathayo David ( wa tatu mbele kulia) akiongozana na kamati hiyo walipofika kwenye kijiji Cha Tukamisasa wilayani Chalinze kukagua miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Baadhi ya wabunge wakiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga ( wa tatu kulia mbele) wakicheza pamoja na wakazi wa kijiji Cha Tukamisasa mara baada ya kuridhishwa na miradi kwenye kijiji hicho. ( Picha zote na Christina Cosmas, Pwani)
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akizungumza na wakazi wa kijiji Cha Tukamisasa juu ya matumizi ya umeme kwa maendeleo mara baada ya kufika kijijini hapo kukagua miradi ya umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).



Na Christina Cosmas, Chalinze


WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imetumia zaidi ya shilingi Trilioni 1.102 kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye Taasisi za Afya 5 na Pampu za maji 16 ambazo hazijafikiwa na huduma ya umeme ili kupambana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo UVIKO-19 mkoani Pwani.

 

Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy amesema hayo wakati akiongea mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge la Nishati lillilotembelea mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa II katika Kijiji cha Tukamisasa kilichopo Tarafa ya Ubena Zomozi Wilayani Chalinze mkoani hapa.

 

Anasema fedha hizo ambazo zimetolewa bila VAT zimefadhiliwa na Serikali ya Tanzania Pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 9 kuanzia Novemba 2022 hadi Oktoba 2023.



Alisema mradi huo unatekelezwa katika Wilaya za Bagamoyo, Kibiti, Mafia, Kibaha, Kisarawe, Mkuranga na Rufiji.



Mhandisi Saidy anasema mradi huo utataekelezwa katika maeneo 21 ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme ambapo hadi kufikia Machi 10 mwaka huu tayari Mkandarasi M/s State Grid Electrical and Technical Worls Limited amekwishatekeleza mradi kwa wastani wa asilimia 60 ya wigo wa mkataba.



Awali mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Tukamisasa Habiba Athumani aliishukuru serikali kwa kuwaingizia umeme na kuomba huduma ya upatikanaji wa umeme kwa wepesi iende sambamba na upatikanaji wa maji na kuwaepushia adha ya magonjwa ya tumbo yanayowakumba mara kwa mara kutokana na kutumia maji wanayotumia Wanyama kwenye marambo tangu nchi kupata uhuru.



Hata hivyo Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema wanajipanga kufanya mapitio ili kuona haki inatendeka kati ya wananchi kutoka vijiji wanaolipa umeme kwa gharama za wakala wa umeme vijijini (REA) na wananchi wanaotoka vijiji miji wanaopaswa kulipa gharama za huduma ya umeme Tanesco ili kuondoa mkanganyiko uliopo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post