Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KWA WADAU KATIKA KUKABILIANA NA MAAFA

 
Mkurugenzi wa Mashirikiano ya Kimkakati kutoka Taasisi ya GSMA Bw. Dulip Tillekeratne akiwasilisha mada wakati wa warsha iliyolenga kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi za ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa Tahadhari ya Awali (Early Warning System – EWS) iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Best Western City Dodoma.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia wasilisho kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa wakati wa warsha iliyolenga kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi za ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa Tahadhari ya Awali (Early Warning System – EWS).

Mkurugenzi Msaidizi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Jane Kikunya akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha iliyolenga kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi za ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa Tahadhari ya Awali (Early Warning System – EWS) iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Best Western City Dodoma tarehe 14 Machi, 2024.

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Mkurugenzi Msaidizi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Jane Kikunya amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau mbalimnali katika masuala ya uratibu wa maafa nchini ili kuendelea kuwa na stahimilivu na maafa. 

Ameyasema hayo wakati akifungua Warsha ya siku moja iliyowakutanisha wadau kutoka Serikalini, Makampuni ya simu, Taasisi zinazotoa Misaada ya kibinadamu kwa lengo la kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi ya ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa tahadhari ya Awali (Early Warning System – EWS) iliyofanyika tarehe 14 Machi, 2024 Jijini Dodoma.

Warsha hiyo ilihudhuriwa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi ikiwemo TCRA, TMA, REDCROSS, makampuni ya simu pamoja na Airtel, Vodacom, Tigo/Zanztel.

Aidha alitumia fursa hiyo kueleza majukumu ya msingi ya Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni kuratibu masuala ya menejimenti ya maafa nchini huku akiwaasa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika mzingo wa menejimenti ya maafa ikiwemo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili pamoja kurejesha hali pindi maafa yanatokea.

“Tumienie warsha hii kwa matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa kuongeza ujuzi na kushirikishana uzoefu katika masuala yanayohusu fursa mbalimbali kuhusu njia sahihi za kutumia teknolojia ya simu katika mifumo na kutoa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kuwa na utayari katika kukabili maafa,” alieleza Bi. Jane

Aliongezea kuwa nchi ya Tanzania imekuwa ikikumbwa na maafa ya asili na yale yasiyo ya asili ikiwemo ya mafuriko, matetemeko ya ardhi, moto, maporomoko ya tope na mawe, ukame, upepo mkali, magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama hivyo warsha hiyo ni muhimu kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kujiandaa kisha kukabili kwa wakati na kupunguza madhara yanayoweza kutokea wakati wa maafa hayo.

Alifafanua kuwa, taarifa za awali zinaipa jamii uelewa wa hatua za awali za kuchukua kabla ya madhara ya maafa kuwa makubwa hivyo upo umuhimu wa kuendelea kuzijengea uwezo jamii juu ya matumizi sahihi ya taarifa hizo.

Awali aliwakumbusha kuendelea kupiga namba 190 endapo kunatokea majanga, maafa au dharura ili kupata msaada zaidi kupitia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com