Na Mwandishi wetu- Dodoma
Serikali kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu inaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino kuanzia Septemba 2023 hadi Juni 2024.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa-Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) Brigedia Hosea Ndagala katika Kikao Kazi cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino Septemba 2023 hadi Juni 2024 ambapo alisema kutokea kwa maafa husababisha madhara ambayo huathiri utendaji kazi, kuzorotesha maendeleo na ukuaji wa kiuchumi kwa wananchi na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu na hivyo, kuzorotesha hatua za maendeleo.
Alisema Maafa hayo yamekuwa yakisabibisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu, na ongezeko la tegemezi kutokana na Watoto kupoteza wazazi.
“Nchi yetu imekuwa ikishuhudia matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii. Maafa haya yamekuwa yakisabibisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu,”Alisema Brigedia huyo.
Aidha Brigedia Ndagala alizitaka kila sekta kuwasilisha tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino ambao una lengo la kuhakikisha serikali na wadau wanachukua hatua stahiki kuzuia au kupunguza madhara na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kutokana na maafa yanayosababishwa na El Nino ili kuokoa maisha na mali.
“Hatua hii ni muhimu ili kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa mvua za Masika. Ni imani yangu kuwa kikao kazi hiki kitatoka na mikakati madhubuti itakayosaidia kuendelea kuongeza ufanisi katika kukabiliana na maafa,” Alieleza.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Social Plugin