TGNP-UWAKILISHI WA WANAWAKE NAFASI ZA UONGOZI BADO CHANGAMOTO


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

TAKWIMU zinaonesha bado hakuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika nafasi za uongozi, za kuchaguliwa au kuteuliwa katika ngazi mbalimbali za uongozi na hata hivyo ukilinganisha na tulipotoka, kuna mabadiliko chanya katika ushiriki wa wanawake na uongozi.

Lengo namba 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu linataka wanawake washiriki kikamilifu na kwa tija na fursa sawa katika uongozi na ngazi zote za maamuzi katika siasa, uchumi na Maisha kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa leo Machi 21, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania- TGNP, Bi. Lilian Liundi wakati akifungua warsha ya waandishi wa habari ngazi ya jamii iliyofanyika katika Ofisi za TGNP Mabibo Jijini Dar es Salaam.

Amesema kutokana na mila na mitizamo kandamizi ambayo inadai kuwa wanawake hawana nafasi kwenye umma, madai yanayopewa nguvu na maarifa duni waliyonayo wanawake na uelewa mdogo wa haki zao,

"Kwa wale waliofanikiwa kuwa viongozi walau katika nafasi ndogo za maamuzi, wamekuwa wakiacha nafasi hizo kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kuungwa mkono (supportive mechanism) kuanzia kwenye ngazi ya familia hadi jamii kwa ujumla". Amesema

Aidha amesema pamoja na kujivunia kuwa na wanawake viongozi katika nafazi za juu za maamuzi katika mihimili miwili ( Serikali na Bunge) pamoja na maeneo mengine, bado kuna changamoto kubwa katika kufikia 50/50.

Ameeleza kuwa bado hakuna mifumo rasmi na wezeshi ya kikatiba , kisheria na kisera, katika usawa katika nafasi za uongozi. Mila kandamizi, desturi na mitizamo hasi dhidi ya ushiriki wa wanawake katika maamuzi bado ni changamoto kubwa katika jamii yetu.

Kwa upande wake Mwandishi wa habari kutoka Rufiji FM, Bi. Kaundime Bakari amesema vyombo vya habari ni vyanzo vikubwa kupeleka taarifa eneo husika, hivyo atatumia chombo chake cha habari kuhakikisha wanatengeneza programu mbalimbali ambazo zinachochea wanawake kushiriki katika uongozi.

"Tunapoelekea kwenye kipindi cha uchaguzi, nitawashawishi wanawake wenzangu kuhakikisha wanashiriki katika kugombea nafasi ya uongozi mbalimbali na wasiweze kukaa nyuma". Amesema

Nae Mdau wa habari nchini, Bw. Meshack Michael amesema licha ya uwepo wa taasisi mbalimbali ambazo zinahimiza wanawake kushiriki katika uongozi, kuna jukumu la muhimu kwa waandishi wa habari nao wakatoa ushirikiano wa kutosha kwa taasisi hizo ili kundi kubwa la wanawake waweze kujitokeza katika kugombea nafasi za uongozi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post