Uongozi wa Chemba ya Biashara ,Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga ukiwa ofisini kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro.
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog .
Uongozi wa Chemba ya Biashara ,Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga umekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro na kujadili mambo mbalimbali kuhusu sekta ya viwanda na ujasiriamali.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo Alhamis Machi 28, 2024, kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga yenye lengo la kujitambulisha na kujadili kwa pamoja masuala ya uwekezaji katika viwanda, biashara na kilimo kwenye wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho kifupi, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro ameupongeza uongozi wa TCCIA mkoa wa Shinyanga kwa kufanya ziara ya kutembelea ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kufahamiana ili waweze kupanga namna watakavyohamasisha wadau mbalimbali kuwekeza katika wilaya hiyo hususani kwenye sekta ya biashara na viwanda.
“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika maendeleo kwa kutoa ajira kwa vijana na kuongeza pato la kiuchumi, kwa kutambua mchango huo serikali itaendelea kuunga mkono jitihada hizo na mimi kama mkuu wa wilaya niwaahidi ushirikiano wakati wote, na niwasihi tuendelee kuhamasisha wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali kuja kuwekeza kwenye wilaya yetu kupitia kilimo, biashara na viwanda kwani bado tuna maeneo makubwa kwa ajili ya uwekezaji”, amesema Wakili Mtatiro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Shinyanga Jonathan Manyama amempongeza mkuu wa wilaya na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Wilaya ya Shinyanga na mkoa kwa ujumla.
Uongozi wa Chemba ya Biashara ,Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga ukiwa ofisini kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akiupongeza Uongozi wa Chemba ya Biashara ,Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akiupongeza Uongozi wa Chemba ya Biashara ,Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga.