WAKALA WA VIPIMO YAANZA KUHAKIKI MITA ZA UMEME


Katika kuendelea kuhakikisha kunakuwa na usawa kwenye matumizi sahihi ya vipimo kama inavyoelekeza Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 taasisi ya Wakala wa Vipimo (WMA) imeanza kufanya uhakiki wa mita za umeme mpya ambazo zinaenda kufungwa kwa wateja katika maeneo mbalimbali ambapo kwa awamu ya kwanza Wakala imepokea jumla ya mita za umeme 500 kupitia kituo chake cha uhakiki wa Vipimo kilichopo Misugusugu Mkoa wa Pwani.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa ameeleza kuwa jumla ya mita za umeme 500 zimepokelewa kutoka kampuni ya CRJE (East Africa) L.T.D ambayo imepata kazi ya kusambaza mita hizo ambazo zinatarajiwa kwenda kufungwa katika mradi wa REA mkoani Geita.

Bi. Stella Kahwa amesema kuwa uhakiki wa mita mia tano (500) za umeme umefanyika kwa muda wa siku moja na mteja kukabidhiwa mita zake. Pia, ameeleza kuwa Wakala ina uwezo wa kupima mita nyingi za umeme kwa kutumia muda mfupi kwakuwa ina mitambo ya kisasa ambapo miwili ipo katika kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu na mmoja upo katika jengo la WMA Mkoani Kilimanjaro.

Katika mita 500 zilizowasilishwa asilimia 95 zimepita kwenye zoezi la uhakiki na zimewekewa rakili (seal) kwa ajili ya kuzilinda zisichezewe na asilimia 5 ya mita hazijaruhusiwa kuingia katika matumizi mpaka zitakapofanyiwa marekebisho na kuletwa tena kwa ajili ya zoezi la uhakiki na endapo zitakidhi vigezo zitaruhusiwa kutumika.

Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa wito kwa wadau wanaopata tenda za kusambaza mita za umeme kuhakikisha mita zao zinaletwa kwa ajili ya uhakiki ili kujiridhisha kama zinapima kwa usahihi kama Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 inavyoelekeza ili kuhakikisha mteja anapata vipimo sahihi katika mita na Shirika la Umeme (TANESCO) linakusanya fedha kulingana na matumizi sahihi ya umeme yanayotumiwa na wateja wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post