Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKUFUNZI KUTOKA NCHI 5 ZA AFRIKA MASHARIKI KUSHIRIKI MAFUNZO YA MFUMO WA USIMAMIZI WA USALAMA WA VYAKULA


MAFUNZO kwa Wakufunzi Kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa Usalama wa Chakula ( ISO 22000) ambayo yameandaliwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) yamefunguliwa jijini Dar es Salaam yakishiriki nchi tano za Afrika Mashariki (EAC).

Mafunzo hayo ya siku nne yanahudhuriwa na wakufunzi utoka nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Somalia, Ethiopia ili kuwezesha bidhaa za chakula kutoka ndani ya nchi hizo kuuzika popote katika masoko ya kikanda.

Aidha, mafunzo hayo yanahudhuriwa na washiriki wengine kutoka Mauritius, India, na Uswisi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungulia kwa mafunzo hayo jana, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athumani Ngenya,  alisema ni heshima kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mafunzo haya, ambayo yanalenga kuwapa wataalamu wa Kiafrika katika sekta ya chakula maarifa na ujuzi juu ya mahitaji na manufaa ya viwango vya usimamizi wa usalama wa chakula.
 
Dkt. Ngenya alisema mafunzo hayo yana faida kubwa kwa sababu viwango hasa vya chakula vina faida kubwa sio tu kwa watumiaji, bali pia kwa wafanyabiashara.

"Bidhaa za chakula zikitengenezwa kwenye hali nzuri na kwa kufuata viwango, basi biashara itaweza kununuliwa nje ya nchi na kuwezesha nchi kukua kiuchumi kupitia viwango," alisema Dkt. Ngenya.  

Kwa msingi huo, Dkt. Ngenya alisema mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuwawezesha washiriki kuelewa viwango hivyo na ku-adapt (kuasili).

"Ni wazi kwamba viwango vya bidhaa zetu za chakula vikiwiana zitaweza kuuzika popote duniani, kwani zitakuwa zimewiana kwa sawa viwango na vile vya kimataifa," alisema Dkt. Ngenya.

Alisema bidhaa zikiwa na utofauti wa viwango itakuwa vigumu kuweza kufanya biashara miongoni mwetu.

"Lakini wote tukiasili (ku-adapt) biashara itakuwa rahisi, kwani mbali ya usalama wa chakula kwa sisi watumiaji, lakini kibiashara itakuwa imeweza kuleta manufaa makubwa sana," alisema Dkt. Ngenya.

Alisema anaelewa usalama wa chakula ni mojawapo ya vipengele muhimu katika ajenda ya usalama wa chakula duniani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com