Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATANZAMIA TUMIENI FURSA KUPELEKA BIDHAA UINGEREZA


-Dkt. Kijaji: Watanzania tumieni fursa kupeleka bidhaa Uingereza.

Serikali imewashauri watanzania kutumia fursa ya mpango wa biashara wa Nchi zinazoendelea kwa kuhakikisha wanapeleka bidhaa katika nchi ya Uingereza ili kukuza Uchumi pamoja na pato la Taifa.

Mpango huo mpya umeanza kutumika mwaka jana 2023 ambapo Serikali ya Uingereza iko tayari kupokea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini zikiwemo zenye kulipiwa ushuru na zisizolipiwa.

Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo leo Dar es Salaam katika semina ya wafanyabiashara kuhusu fursa ya kuuza bidhaa katika soko la Uingereza na Nchi zinazoendelea (UK- DCTS).

Akizungumza Mhe.Dkt. Kijaji amesema mpango huo wa bishara na Nchi zinazoendelea kwa Tanzania umekuja muda muafaka kwa kuwa Nchi imerekebisha na kuboresha mazingira ya biashara ili kufanya kukuza kipato na biashara nchini.

Amesema kwa mwaka 2022 mauzo ya Tanzania kwenda Uingereza yalifikia sh. bil 44 ikilinganishwa na manunuzi ya sh. trilioni 3.08 ya bidhaa kutoka Uingereza.

Amesema kupitia takwimu hizo ongezeko la mauzo kwenda Uingereza ni ndogo sana ikilinganishwa na ununuzi wa bidhaa kutoka Uingereza Kwenda Tanzania kwani kwa miaka miwili imeongezeka sh. bilioni mbili wakati bidhaa zilizonunuliwa ni zenye thamani ya sh. triloni 1.06.

“Inahitaji nguvu ili kuweza kuvuka na kufikia malengo halisi ya kuanzishwa kwa mpango huo,” amesema Waziri Kijaji.

Aidha, ametolea mfano taarifa ya Kituo cha Uwekezaji nchini ( TIC) kuanzia mwaka 1997-2024 jumla ya miradi 980 ya kampuni ya Uingereza yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5655.38 zilizotoa ajira za wastani wa watu 126,322 katika sekta mbalimbali ziliwekezwa nchini.

“ Tuweze kutumia mpango huo na kuchochea mapato pamoja na fedha za kigeni, lakini pia kupitia mpango huo Taifa litakuwa na manufaa mbalimbali ambayo ni kupungua kwa masharti ya kupeleka bidhaa na kwa wenye viwanda ni muhimu kuwa na malighafi zitakazochochea ushindani wa bidhaa za Tanzania,” amesema.

Ameongeza pia manufaa ya mpango huo ni kupungua kwa gharama za kufanya biashara kurahisisha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa Tanzania na hata kushirikiana na kampuni za Uingereza kuwekeza na kuzalisha bidhaa bora Tanzania.

Amehamasisha wafanyabiashara kuona umuhimu wa uadilifu katika kuziona fursa na kwamba wapeleke bidhaa zinazokidhi soko hilo.

“Serikali yetu ya awamu ya sita imechukua hatua nyingi za kujenga mahusiano ya kidipolomasia na Uingereza ambapo Nchi hiyo pia ilianza kutoa fedha kupitia huduma mbalimbali ambazo zimeelekezwa katika Miradi mbalimbali,” amesema.

Mhe. Dkt.Kijaji ameongeza kuwa mpango huo umezingatia pia sekta ya biashara kwa kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika ukuaji wa viwanda.

Akitoa ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania David Cancar amesema chini ya mpango huo Tanzania ndio yenye bidhaa zinazotakiwa na Uingereza.

Amesema kupitia mpango huo kwa Pamoja kutakuwa na ongezeko kubwa la biashara kati ya Tanzania na Uingereza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com