Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Shinyanga (TAKUKURU) kupitia Program ya TAKUKURU RAFIKI imesaidia kutatua kero za wananchi mkoani Shinyanga.
Akitoa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za TAKUKURU kwa kipindi cha robo ya tatu ya Januari hadi Machi 2024 leo Jumanne Aprili 23,2024 Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amesema Programu ya TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa majibu ya kero ya kutopimwa maeneo ya makazi kwa wananchi wa kata ya Ndala Mtaa wa Ndala tangu mwaka 2018.
“Awali wananchi zaidi ya 246 walichanga kiasi cha shilingi 12,396,000/= na kulipa Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya zoezi la upimaji ardhi. Pia wananchi 1150 wa mtaa wa Mlepa waliokuwa wamechanga fedha kwa ajili ya kupimiwa na kurasimishiwa maeneo yao lakini walikuwa bado hawajapatiwa namba za upimaji wa viwanja vyao tangu mwaka 2023 walipopimiwa”,amesema Kessy.
“Wananchi wa mtaa wa Ndala walitoa keto yao kutopimiwa na kurasimishiwa maeneo yao pamoja na kuwa walikwishachangia huduma hiyo tangu mwaka 2018. Vilevile wananchi wa mtaa wa Mlepa kero yao ilikuwa kupatiwa namba za viwanja vyao tangu walipopimiwa mwaka 2023”,ameeleza.
Amesema hali hiyo ilikuwa inapelekea migogoro ya mipaka, kuwanyima fursa ya kupata mikopo katika taasisi za kifedha kwa kutumia ardhi kama dhamana lakini pia viwanja kutoongezeka thamani kwa kukosa utambuzi rasmi.
“Baada ya kupokea kero hiyo, TAKUKURU iliwasilisha Manispaa ya Shinyanga bango kitita lenye kero kusika na mikakati ya utatuzi wa kero hiyo. Halmashauri ya Manispaa Idara ya ardhi walishughulikia kero hiyo ambapo katika mtaa wa Mlepa zoezi la kugawa namba za viwanja lilianza na hadi sasa namba za viwanja 412 zimeanza kugawiwa tangu mwezi Januari na zoezi bado linaendelea”,amefafanua Kessy.
“Mwezi Februari Manispaa ya Shinyanga ilifanya zoezi la upimaji katika mtaa wa Ndala na kwa sasa Manispaa ipo kwenye mchakato wa ukamilishaji wa utengenezaji wa ramani kwa ajili ya kusajiriwa Wizarani na baada ya hapo kupata namba za viwanja hivyo 246 vya wananchi wa mtaa wa Ndala”,ameongeza.
Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga amesema TAKUKURU inaendelea kufuatilia ugawaji wa namba za viwanja vilivyopimwa katika mtaa wa Mlepa mpaka litakapokamilika lakini pia kufuatilia zoezi la ukamilishaji wa uandaaji wa namba za viwanja za mtaa wa Ndala na ugawaji wake.
Hali kadhalika TAKUKURU inaendelea kufanya vikao vya utambuzi wa kero katika kata 14 kutoka kata za Mwenge, Mwawaza, Kolandoto, Lyabukande, Puni, Nyida, Mhongoloi, Majengo, Nyasubi, Ulowa, Bulungwa, Mpunze, Bupigi na Bubiki.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari
Social Plugin