Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BUTONDO AKABIDHI EKARI 180 KWA WAKAZI WA IKONDA A ZILIZOKUWA ZIKIMILIKIWA NA TFS



Na Mwandishi Wetu - Kishapu

Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga (CCM) Mhe. Boniface Butondo amekabidhi ekari 180 kwa Wakazi wa Kijiji cha Ikonda A kata ya Mwaweja kutoka Wakala wa Mistu Tanzania (TFS) kati ya ekari 247 ambazo awali zilikuwa zikihifadhiwa na Wakala huo.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 1,2024 Mhe. Butondo amesema Serikali ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wamekubaliana kuimega hifadhi ya Misitu Ikonda ekari 180 na kuzirejesha kwa wananchi huku ekari 67 pekee zikibaki kwa Wakala huo kwaajili ya kuhifadhiwa.

“Mhe. Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi viongozi tutatue migogoro ya Wananchi na sisi leo tumetekeleza agizo hili kwa vitendo, nikiwa Mwakilishi wa Wannchi wa Jimbo la Kishapu kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa wilaya na TFS Kishapu ninawakabidhi wananchi ekari 180 ili waendelee na shughuli za kilimo na Ufugaji,”amesema Butondo.
Sambamba na hilo Butondo amewataka TFS kuweka mipaka inayoonekana ikiwemo alama (BIKON) katika eneo la ekari 67 ili kuzuia kutovamiwa na kuwataka Wananchi kuheshimu maamuzi ya serikali kwa kutumia eneo lao la ekari 180 kwa ajili ya Kilimo na Ufugaji.

Kwa upande wake, Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kishapu Tumain Masatu amewapongeza wakazi wa Kijiji cha Ikonda A kwa kuwa watulivu kwa muda mrefu wakati wa utatuzi wa mgogogoro huo ambao umepatiwa suluhu kwa kupatiwa ekari 180 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kilimo na ufugaji.

“Wananchi Suala la Uhifadhi tusilichukulie kama ni uadui,tuendelee kudumisha Mahusiano na tushiriki katika kutunza mazingira kwa kulinda maeneo yaliyohifadhiwa kama Serikali inavyoelekeza,hizi ekari 67 ambazo zinaendelea kuhifadhiwa na TFS tuzilinde,”amesema Masatu.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Kishapu Fadhili Mvanga amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassani ni Sikivu na inasikiliza wananchi ikiwa ni Pamoja na kutatua kero zao,hivyo Wakazi wa Kijiji cha Ikonda A wamerejeshewa ekari hizo ili waziendeleze kwa kilimo na ufugaji.

Awali akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu aliwataka Wananchi kuiamini serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ,kwa kuwapenda wananchi wake ikiwa ni Pamoja na kutatua kero zao ikiwemo ya misitu.

Mmoja wa Wakazi wa Kijiji cha Ikonda A Nkelebi Masanja ameipongeza Serikali kwa kutatua mgogoro huo ambao umedumu kwa muda wa miaka mitano,na kurejeshwa kwa ekari hizo 180 kutawawezesha kujikwamua kiuchumi kwa kutekeleza shughuli za kilimo na ufugaji.

“Tunaahidi kulitumia eneo hili kwa matumizi stahiki,na hatutavamia eneo la TFS,tutakuwa mabalozi wa ujirani mwema katika uhifadhi na kamwe hatutakata miti yote katika eneo hilo ambalo tumekabidhiwa leo,”amesema Masanja.

Mwaka 2018 Jumla ya Ekari 247 zilizokuwa zikimilikiwa na Hifadhi ya Vijiji Shinyanga (HVS) lilikabidhiwa kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kishapu na kusababisha mgogoro baina ya Wananchi kwa kile kilichodaiwa baadhi ya maeneo ya wananchi yalichukuliwa kimakosa.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga (CCM) Mhe. Boniface Butondo akizungumza wakati akikabidhi ekari 180 kwa Wakazi wa Kijiji cha Ikonda A kata ya Mwaweja kutoka Wakala wa Mistu Tanzania (TFS) kati ya ekari 247 ambazo awali zilikuwa zikihifadhiwa na Wakala huo.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com