Wizara ya Kilimo imekuwa na mkakati wa kutoa mafunzo kuhusu Mfumo wa Crop Stocks Dynamics System (CSDS) kwa watalaamu wa kilimo katika ngazi ya Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa ili kuimarisha usalama wa chakula na upatikanaji wa masoko nchini.
Huu ni mfumo wa kidigitali wa kusajili ghala, masoko, vituo vya ukaguzi wa mazao na wafanyabiashara ili kufuatilia uhifadhi wa mazao ya kilimo kwenye ghala, usafirishaji wa mazao ya kilimo na ufuatiliaji wa mazao yanayoingia kwenye masoko ya walaji. Mfumo huu una sehemu tatu ambazo ni Usimamizi wa mazao ya kilimo kwenye ghala, Usimamizi wa mazao ya kilimo yanayoingia sokoni na Ufuatiliaji wa mazao ya kilimo yanayosafirishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Mfumo huu unaosaidia kutoa taarifa za usajili wa masoko, ghala na vituo vya ukaguzi wa mazao ya kilimo unawezesha kufahamu takwimu sahihi za kiasi cha mazao yanayoingia na kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Pia mfumo huu unasaidia kukusanya taarifa za bei za mazao ya kilimo katika kila mkoa; na unasaidia kuweza kufahamu kiasi cha hifadhi ya chakula katika kipindi husika hapa nchini kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kisera.
Social Plugin