RC MACHA UZINDUA KAMPENI YA CHANJO SARATANI MLANGO SHINGO YA KIZAZI -HPV KWA WASICHANA SHINYANGA

 


Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amezindua Rasmi kampeni ya utoaji Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi (HPV) kwa wasichana,huku akitoa onyo kwa atakae bainika kufanya upotoshaji juu ya Chanjo hiyo Serikali itamchukulia hatua.

Uzinduzi wa utoaji Chanjo hiyo HPV umefanyika leo Aprili 22,2024 katika Shule ya Msingi Ndala “A” Manispaa ya Shinyanga ambayo itawafikia Wasichana 198,865 wenye umri wa kuanzia miaka 9-14 ili kuwakinga dhidi ya Ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi.
Macha akizungumza kwenye uzinduzi huo, ametoa wito kwa wazazi kuwaruhusu Watoto wao wapatiwe Chanjo hiyo ya (HPV) ili kuwakinga dhidi ya Ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi, huku akiwaonya wale ambao watapotosha juu ya Chanjo hiyo Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria.

“Chanjo hii ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi ni salama kabisa na haina madhara yoyote, na ilianza kutolewa tangu mwaka 2014, na tangu kipindi hicho hakuna madhara yoyote ambayo yametokea, sasa kwa wale ambao wataanza upotoshaji Serikali itawachukulia hatua,”amesema Macha.
“Mwananchi yoyote ambaye hana uelewa vizuri dhidi ya Chanjo hii, ni vyema akafika kwenye huduma za Afya au maeneo ambayo Chanjo inatolewa mashuleni, aulize na kuelimishwa kuliko kuanza kuandika kwenye Mitandao ya Kijamii na kufanya upotoshaji au kwenye vijiwe, tukikubaini tutakuchukulia hatua,”ameongeza Macha.

Aidha, amesema Serikali haiwezi kuleta Chanjo yenye madhara kwa wananchi wake ambapo Chanjo hiyo imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), na kuwataka wazazi wasiwe na wasiwasi dhidi ya Chanjo hiyo.
Amewataka pia Walimu pamoja na Wataalamu wa Afya, kwamba zoezi hilo la Utoaji Chanjo katika maeneo ya Shule lipangiliwe vizuri, ili lisiweze kuharibu vipindi vya masomo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa, ametoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kwamba wajenge utaratibu wa kupima Afya zao mara kwa mara, ili kujikinga dhidi ya Magonjwa mbalimbali, na siyo kusubili magonjwa hayo kuwa sugu au kupelekwa hospitali wakiwa hoi
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk,Yudas Ndungulile, amesema tayari Chanjo zote zipo kwenye Vituo, ambapo zitatolewa katika maeneo ya Shule za Msingi na Sekondari, pamoja na kwenye Vituo vya Afya, na watawafikia wasichana 198,865 wenye umri wa kuanzia miaka 9-14 na watapewa Dozi Moja tu.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Shadrack Geofrey, ameupongeza Mkoa wa Shinyanga kwa kufanya Maandalizi Mazuri ya Utoaji wa Chanjo hiyo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi HPV, kwamba ametembelea Halmashauri zote na kujiridhisha maandalizi yapo vizuri.
Mmoja wa wazazi Rose Mathias, ameishukuru Serikali kwa kutoa Chanjo hiyo na kuwalinda watoto wao, na kutoa wito kwa wazazi wawa ruhusu Mabinti zao wapatiwe Chanjo hiyo, na kwamba Watoto wa kike huwa wanakabiliwa na Magonjwa mengi.

Naye Mwanafunzi Amina Hassani ambaye amepatiwa Chanjo hiyo ya HPV,amesema amefarijika kuchomwa Chanjo ambayo itamlinda dhidi ya Ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi HPV,Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, akimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro kwenye uzinduzi wa Chanjo hiyo ya HPV.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudasa Ndungile akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni hiyo ya utoaji Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi HPV Mkoa wa Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dk.Elisha Robert akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni hiyo ya utoaji Chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 9-14.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Shadrack Geofrey akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Utoaji Chanjo ya HPV kwa Wasichana Mkoani Shinyanga.
Mwakilishi kutoka TAMISEM Paul Julius akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Utoaji Chanjo ya HPV kwa Wasichana Mkoani Shinyanga.
Mzazi Rose Mathias akiishukuru Serikali kwa kuwapatia Chanjo ya HPV Watoto wao na kulinda dhidi ya Ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Shingo ya Kizazi.
Mwanafunzi Halima Saidi akiishukuru Serikali kwa kuwapatia Chanjo hiyo ya HPV ili kuwalinda dhidi ya Ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Shingo ya Kizazi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizundua Rasmi Kampeni ya Utoaji Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi HPV kwa wasichana mkoani humo wenye kuanzia umri wa miaka 9-14.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akimpatia Kadi Mwanafunzi Amina Hassan mara baada ya kuchanjwa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi.
Muunguzi wa Zahanati Masekelo Onesmo Mwamfupa akimchoma Chanjo ya HPV Mwanafunzi Amina Hassan mara baada ya Mkuu wa Mkoa kumaliza kuzindua Kampeni hiyo.
Mwakilishi kutoka TAMISEM Paul Julius akimpatia Mwanafunzi Chanjo ya HPV ili kulinda dhidi ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya Kizazi.
Wanafunzi wakiwa kwenye uzinduzi wa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi HPV.
Wanafunzi wakiwa kwenye uzinduzi wa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi HPV.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Shinyanga Timoth Sosoma akiwa kwenye uzinduzi wa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi HPV.
Uzinduzi wa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi ukiendelea.
Uzinduzi wa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi ukiendelea.
Uzinduzi wa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya kizazi ukiendelea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post