WATUHUMIWA 12 WA KILO 726.2 ZA DAWA ZA KULEVYA WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Watuhumiwa watatu wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Mkoani Pwani jana tarehe 22 Aprili, 2024  wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Methemphetamine Kilogramu 424.84 pamoja na Heroin Hydrochloride gramu 158.24 kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) na cha (3) (i) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 kama illivyorejewa 2019. 

Washtakiwa hao ni Rajabu Kisambwanda (42) mkazi wa Kerege Matumbi, Bakari Said (39) Mkazi wa Kunduchi Mtongani na Hillary Rhite (35) Mkazi wa Kunduchi Sodike.

Wakisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Mkhoi na Wakili wa Serikali, Agness Ndanzi, alidai mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao watatu walikutwa wakisafirisha dawa hizo za kulevya mnamo tarehe 10 Aprili, 2024 eneo la Zinga wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani .

Wakili Ndazi aliendelea kuieleza Mahakama kuwa, katika tukio lingine, tarehe hiyohiyo mshtakiwa Bakari Said (39) Mkazi wa Kunduchi Mtongani alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin hydrochloride yenye uzito wa gramu 158.24.

Hata hivyo washtakiwa wote watatu hawakuruhusiwa kujibu chochote kwani Mahakama hiyo haina Mamlaka ya kisheria kusikiliza shauri hilo na watafikishwa tena mahakamani kwa ajili ya kutajwa tarehe 7 mwezi Mei, 2024.

Katika tukio lingine, watuhumiwa wengine tisa (9) wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana tarehe 22 Aprili, 2024 wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine zenye uzito wa kilogramu 332. 

Akisoma mashtaka yao mbele ya mahakama hiyo, wakili wa serikali Batilda Mushi amewataja washtakiwa hao kuwa ni Ally Ally @kabaisa (28), Bilali Hafidhi (31), Mohamed Hamisi (47), Idrisa Mbona (33), Rashid Rashid (24), Shabenga Shabenga (24), Dunia Mkambilah (52), Mussa Hussein (35) na Hamis Omary (25). 

Amesema, katika shtaka la kwanza, tarehe 16 Aprili, 2024 karibu na hotel ya white sands wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine kiasi cha kilgramu 100.83.

Katika shtaka la pili wakili Mushi amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Richard Kabate kuwa, tarehe hiyohiyo, karibu na eneo la hotel ya white sands wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin hydrochloride kiasi cha kilogramu 232.69 kinyume na kifungu namba 15 (1|) (a) nq (3) (i) cha sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 kama ilivyorejewa mwaka 2019, ikisomwa pamoja na aya ya 23 jedwali la kwanza kifungu namba 57 (1|) na 60 (2)  cha Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 ya mwaka 2022.

Hata hivyo, washtakiwa wote hawakuruhusiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwani Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri hilo.  Aidha, upande wa mashtaka uliieleza mahakama hiyo kwamba upelelezi wa shauri bado unaendela na kuomba kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa ambapo Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 6 Mei, 2024. 

Washtakiwa wote wamerudishwa mahabusu kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Watuhumiwa  waliofikishwa Mahakamani ni kati ya watuhumiwa 21 waliotangazwa na kamishna jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya tarehe 22 April, alipozungumza na waandishi wa habari kufuatia ukamataji wa kilo 726.2 zilizokamatwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post