Na WAF, GEITA
Kambi ya madaktari bingwa wa mama Samia waliopo Geita imetajwa kuwa kichocheo cha utoaji wa huduma bora za matibabu katika mkoa wa Geita.
Hayo yamesemwa leo Aprili 29, 2024 na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Martin Shigela wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Kambi ya Madaktari Bingwa na Bobezi waliopo mkoani hapo kwa ajili ya kushughulikia magonjwa mbalimbali ikiwemo kuwafundisha ujuzi wataalam wa mkoa huo.
Mhe. Shigella amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada anazozichukua katika kuimarisha huduma za Afya nchini ikiwemo kutoa ufadhili wa kusomesha wataalam na wataalam wabobezi ili waweze kutoa huduma zitakazokidhi mahitaji ya wananchi.
"Ndani ya kipindi cha muda mfupi Rais Samia ameibadili kabisa Sekta ya Afya kwa kuweka miundo mbinu lakini kama haitoshi ametoa ajira zaidi ya 500 katika mkoa wa Geita lakini kama haitoshi leo amewatuma zaidi ya Madaktari 30 kuja kusaidiana na wa hapa Geita kutoa tiba kwa magonjwa ya ndani na hata Saratani". Amesema Shigella.
Aidha, Mhe. Shigella amesisitiza kuwa kama una vifaa na huna Madaktari Bingwa na Bobezi hiyo huduma inakuwa haina maana, lakini Dkt. Samia ametuletea Huduma za Mkoba ambazo ni chachu ya kuboresha huduma nchini.
Katika hatua nyingine Mhe. Shigella, amewashukuru wananchi wa Geita kwa kujitokeza kwa wingi kwenye kambi hiyo itakayodumu kwa siku tano.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuzungumza na hadhara iliyohudhuria ufunguzi huo, Katibu Tawala mkoa wa Geita Robert Gombati, amesema uwepo wa Madaktari Bingwa na Bobezi kwao ni kichocheo cha wananchi wengi kwenda kupata huduma.
"Huduma hii ya Mkoba, endapo ingekuwa Bugando, Ocean Road au sehemu nyingine yoyote ingekuwa ni gharama lakini leo chini ya Wizara ya Afya huduma hii imewafikia wananchi wetu hapa Geita, kwakweli tunakila sababu yakuishukuru Serikali kutukumbuka wana Geita.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita, Omary Sukari amesema kambi hiyo ni miongoni mwa kambi Sita zitakazo kwenda kote nchini kwa nyakati tofauti na kuangalia magonjwa ya matatizo ya Wamama na watoto, upasuaji, ataangalia magonjwa ya Ndani kama Moyo, Kinywa na Masikio,
Akizungumza kando ya hafla hiyo Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Geita Dkt. Kibwana Mfaume amesema wanatarajia kuwafikia wananchi wasio pungua 3000 ikiwa ni wastani wa wagonjwa 500 kwa siku.
Madaktari Bingwa na Bobezi wa Samia Suluhu Hassan wanaotembea na Kauli mbiu isemayo, Tumekufikia Karibu Tukuhudumie wapo mkoani humo kuanzia Aprili 29 hadi Mei 03, 2024 kwa ajili ya kutoa huduma.