TAKUKURU YABAINI DOSARI MIRADI 21 KAGERA

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera Pilly Mwakasege akizungumza na waandishi wa habari 

 Na Mbuke Shilagi _ Bukoba.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Kagera  imebaini miradi 21 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni  nane kati ya miradi 24 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tisa kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho.


Akitoa taarifa ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia Januari mpaka Machi 2024 Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera ,Pilly Mwakasege amesema kuwa miradi iliyofuatiliwa ni ya ujenzi wa miundombinu ya maji,barabara ujenzi wa zahanati,shule,madarasa,matundu ya vyoo pamoja na bweni na bwalo katika shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa enaendana na thamani ya fedha iliyotumika.


Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi za TAKUKURU Manispaa ya Bukoba Aprili 24,2024 amesema kuwa mapungufu hayo yaliyohitaji marekebisho sawa na asilimia 98.87 ya fedha za miradi iliyofatiliwa kumekuwa na ongezeko la asilimia 30.37 ya fedha za miradi iliyobainika kuwa na mapungufu katika utekelezaji wake kwa kulinganisha na kipindi cha Oktoba - Desemba 2023 miradi iliyofatiliwa na kubainika kuwa na mapungufu ilikuwa asilimia 68.50.


Aidha amesema katika kipindi cha miezi mitatu TAKUKURU imepokea malalamiko 110 kati ya hayo malalamiko 96 hayahusu rushwa hivyo walalamikaji walielimishwa na kupewa ushauri huku malalamiko 14 yalihusu rushwa na kufunguliwa majalada ya uchunguzi na malalamiko 10 kati ya hayo 14 yamekamilika na hatua mbalimbali zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa na mengine manne uchunguzi wake bado unaendelea.

Mashauri mapya nane yamefunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya mashauri 27 yanayoendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali Mkoani Kagera na katika kipindi hicho mashauri tisa yamefanyiwa maamuzi ambapo Jamhuri imeshinda mashauri yote tisa.


Sambamba na hayo amesema katika kipindi cha April - June 2024 wameweka vipaumbele vitakavyolenga kuzuia vitendo vya rushwa visitokee ikiwa ni kuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya ufujaji wa fedha za umma laiki pia kutatua kero mbalimbali kwenye jamii kupitia Program ya TAKUKURU RAFIKI na kufanya chambuzi za mifumo hasa katika maeneo yanayolalamikiwa zaidi na wananchi ili kuboresha na hatimaye kuondoa mianya ya rushwa inayotokana na mifumuko ya utendaji.


Pilly Mwakasege amewahimiza na kuwataka wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuwa waadilifu na kuhakikisha kuwa fedha zote za miradi ya maendeleo zinatumika vizuri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post