Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kinawakumbusha wazazi na walezi kuendelea kuwalinda na kuhakikisha usalama wa watoto wao kueleekea katika sikukuu za Eid el Fitr.
Ikiwa tunaingia katika kipindi cha Sikukuu, tunayo furaha kubwa kuungana na jamii katika sherehe hizi za kipekee. Lakini pamoja na furaha hii, TAMWA ZNZ tunaikumbusha jamii kutosahau majukumu yetu katika kulinda na kuhakikisha usalama wa watoto wetu.
Hivi karibuni tumeendelea kushuhudia ongezeko la matukio ya udhalilishaji, kutoka matukio 1360 mwaka 2022 hadi matukio 1954 mwaka 2023, ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 43.7, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Mtakwimu Mkuu ambayo pia inaonesha kuwa waathirika wengi wa matukio haya ni watoto ambapo kwa mwaka 2023 walikua ni asilimia 83.7 ya waathirika wote.
Kutokana na ripoti hiyo tunasisitiza umuhimu wa kuongeza jitihada za hali na mali katika kupunguza matukio hayo kwa kuwa nao karibu na kuzifuatilia nyenendo za watoto/ vijana wao kwa kipindi chote cha sherehe hizo.
Tunatambua pia umuhimu wa kulinda na kudumisha maadili hasa katika upande wa mavazi na mienendo kwa lengo la kuhakikisha usalama wa watoto wetu. Kipindi hiki cha sikukuu ni fursa ya kipekee ya kuzingatia maadili haya na kuiweka jamii yetu katika mstari unaofaa.
Tunatoa wito kwa kila mwanajamii kuchukua jukumu lake katika kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto wetu na jamii yetu kwa ujumla. Tunapoelekea kusherehekea Sikukuu ya Eid el Fitr, tunawatakia kila la kheri na furaha tele.
Dkt. Mzuri Issa,
Mkurugenzi,
TAMWA ZNZ.