Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Aliyekuwa baba Askofu wa kanisa takatifu katoliki la Orthodox Askofu Dkt. Francis Laurent Bukombe amesimikwa rasmi kuwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo Tanzania.
Sherehe hiyo ya kusimikwa Uaskofu imefanyika leo Aprili 27, 2024 imeambatana na uzinduzi wa jengo la kanisa takatifu katoliki la Orthodox lililopo Kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga.
Awali akizungumza wakati wa zoezi hilo Askofu Mkuu wa kanisa katoliki la Orthodox Askofu Mkuu Dkt. George Jamba amemsihi kuendelea kutoa huduma kwa watu wa aina zote bila upendeleo .
"Mimi kama Askofu Mkuu nimekubali Baba Askofu Francis Laulent Bukombe kuwa Askofu wa kanisa hili na leo namtangaza mbele ya umati na waumini wa kanisa katoliki la Orthodox hapa Tanzania, mtumishi anatolewa katikati ya watu na kurudishwa kwa watu, Yesu Kristo alikuja na akawatawadha wafuasi wake ambao walikuwa na shughuli mbalimbali, Yesu aliwaita wakaitika, wito wa Yesu Kristo hata ukiwa nani ni lazima uitike akikuita", amesema Askofu Mkuu Dkt. George Jamba
"MUNGU ametupatia jukumu la kutoa huduma kwa kila mmoja bila upendeleo wowote hivyo nenda kawatumikie watu wa aina yote, nitakupaka mafuta kichwani pamoja na kukuvalisha mavazi kama ishara ya kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa kanisa takatifu katoliki la Orthodox Tanzania", ameongeza Askofu Mkuu Dkt. George Jamba.
Akizungumza mara baada ya kusimikwa kuwa Askofu wa kanisa hilo Baba Askofu Dkt. Francis Laurent Bukombe ameahidi kutumikia vyema nafasi hiyo na kushirikiana na serikali katika kupinga vitendo vya ukatili pamoja na kuinga ndoa za jinsia moja .
"Leo hii nimepokea jukumu hili naahidi kutumikia vyema
kama vile MUNGU atakavyoniongoza, nishukuru sana wa wale wote waliojitokeza
siku ya leo kushuhudia yale yaliyotendeka katika madhabahu hii, niwaombe
tuendelee kushirikiana, mimi kama kiongozi wa kanisa hili niseme tu tutaendelea kushirikiana na serikali
katika kukemea na kutokomeza matukio na vitendo vya ukatili kwenye jamii,
ubakaji na ulawiti nitasimama kwa nguvu zangu zote kama Askofu kupinga vitendo
hivyo”, amesema Askofu Dkt. Francis Laurent Bukombe.
“Nitapinga ukatili kwa watoto vipigo na udhalilishaji kanisa
litaendelea kupinga na kuhakikisha malezi bora kwa watoto na jamii kwa ujumla,
lakini pia hatutakuwa tayari kubariki ndoa ya jinsia moja, kanisa letu linapinga
kwa nguvu zote ndoa ya jinsia moja kama Askofu sitakubali vitu vya namna hiyo”,
ameongeza Askofu Dkt. Francis Laulent Bukombe.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini
Mhe. Patrobas Katambi amempongeza Askofu Francis Laurent Bukombe kwa kusimikwa
kuwa Askofu wa kanisa hilo.
“Hongera sana kwa mambo makubwa ambayo yametendeka kaika
madhabahu hii, matunda uliyoyazaa ni ushuhuda wa watu uliyowaita hapa, mengi
ulikumbana nayo lakini leo MUNGU amekuinua na kukuchagua wewe kuongoza kanisa
hili, ulipo na imani kwa neno litakuwa”, amesema Mhe. Katambi.
Mbunge wa Viti maalum Shinyanga Mjini Mhe. Christina Mzava akizungumza wakati wa sherehe hiyo.
Zoezi la kusimikwa uaskofu likiendelea.
Social Plugin