Na Mbuke Shilagi Bukoba.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wamefanya maandamano ya amani Aprili 22,2024 katika Mkoa wa Kagera wilaya ya Bukoba ambapo katika Kanda ya ziwa Victoria maandamano yameanzia Mkoa wa Kagera wilaya ya Bukoba na kuongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa Mh. Freeman Mbowe.
Maandamano hayo yamefanyika kwa kutembea na miguu kuanzia kata ya kashai ndani ya mtaa wa Mafumbo wakiwa na mwenyekiti wa CHADEMA Taifa akiwa pamoja na viongozi mbalimbali ngazi ya Kanda ya ziwa Victoria pamoja na viongozi wa Mkoa, Wilaya Kata Mitaa pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali mpaka uwanja wa Mayunga katika kata ya Bilele ambapo waliweza kuweka mkutano na kuzungumza na wananchi wa Kagera.
Aidha maandamano hayo yalikuwa ni kutaka kurekebishwa kwa mambo mbalimbali ndani ya serikali ambapo mabango yaliyobebwa na wananchi yalikuwa yameandikwa "Mfumuko wa bei za vyakula twafa" "bila haki hakuna amani" "Tunataka katiba mpya na tume ya uhuru ya uchaguzi" pamoja na mabango mengine mengi ambayo yalikuwa yanataka kupewa haki ambazo wamedhulumiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Taifa Mh. Freeman Mbowe amesema hakuna jambo linaloweza kuongeza hisia na mtazamo zaidi ya maandamano na kwamba maandamano siyo jambo la mzaha kwa sababu sio kila chama Cha siasa kinaweza kufanya maandamano maana maandamano ni ushawishi na ni turufu ya Chadema.
Pia amelipongeza jeshi la polisi Mkoa wa Kagera kwa kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha kwamba maandamano yanakuwa yenye amani lakini pia kwa kuwa nao pamoja kwa ajili ya kulinda amani bega kwa bega.
Amesemavmaandamano hayo yataendelea ndani ya Kanda ya Ziwa Viktoria katika wilaya nyingine pamoja na Taifa kwa ujumla mpaka pale serikali itakapofanyia kazi kwa yote yanayotakiwa.
Amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kupeleka ujumbe wa sauti zisizosikika ziweze kufika.
"Maandamano ni ujasiri na maandamano ni ukakamavu" ,amesema Mbowe.