Kuelekea Mei 2 & Mei 3, 2024 tarehe za Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kusomwa na kujadiliwa Bungeni Dodoma, Wizara ya kilimo imeangazia faida atakazopata mkulima kwa kufanya kilimo kwa kutumia zana bora za Kilimo na Teknolojia ya kisasa.
Wizara hiyo imeweka bayana kuwa kutumia zana za kilimo katika uzalishaji wa mazao kutamuwezesha mkulima kufanya kazi zake kwa wakati kulingana na msimu wa uzalishaji hivyo kuongeza tija na kupunguza upotevu wa mazao kabla na baada ya kuvuna.
Aidha matumizi endelevu ya mashine za uongezaji thamani mazao ya kilimo kwa kiasi kikubwa yanachangia kuongeza ubora na thamani ya mazao ya kilimo wakati wakulima wakisubiri soko zuri litakalowasaidia kurudisha gharama za uzalishaji na kupata faida kulingana na uwekezaji waliofanya.
Vilevile Matumizi ya zana bora za kilimo huwawezesha wakulima kulima maeneo makubwa kwa haraka na ufanisi zaidi hivyo kuwahi misimu mifupi ya mvua. Hii inawezesha kuzalisha mazao mengi zaidi na kumuongezea mkulima kipato na kupunguza umaskini na kupata uhakika wa chakula.
Hata hivyo matumizi endelevu ya teknolojia za kisasa na zana za kilimo hasa matrekta na zana zingine huchochea sekta binafsi kuanzisha vituo vya kutoa huduma za zana za kilimo, karakana, viwanda vidogo na kati kwa ajili ya kutoa huduma ya matengenezo, vipuri pamoja na kuunganisha matrekta madogo na makubwa hivyo kutoa fursa za kuongeza ajira kwa vijana wa mijini na vijijini.
Social Plugin