Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CRDB BANK FOUNDATION, SUGECO KUWEZESHA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WAHITIMU 2,500 NJE YA NCHI


Katika kufungua fursa za kuongeza umahiri katika fani zao, Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative (SUGECO) imesaini mkataba wa miaka mitatu kuwawezesha zaidi ya wahitimu 2,500 wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa taasisi yake imekuwa ikitekeleza Program ya Imbeju inayotoa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mtaji wezeshi kwa vijana na wanawake.
Tangu walipofungua dirisha la maombi mwaka mmoja uliopita, vijana 709 walijitokeza na kati yao, asilimia 40 kati yao walitoka katika sekta ya kilimo ambayo inaongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni huku ikilihakikishia taifa chakula cha kutosha kwa mwaka mzima.


Kwa kushirikiana na wabia, Tully amesema kilimo kinapewa msisitizo zaidi kwa kutambua mchango wake katika kuliingizia taifa fedha za kigeni, kutoa ajira kwa Watanzania pamoja na kuihakikishia Tanzania usalama wa chakula.
“SUGECO ni mbia wetu mpya katika uwezeshaji wa vijana hasa wanaojihusisha na kilimo. Kwa kutambua umuhimu wa mafunzo kwa vitendo katikakuwajengea uwezo vijana, CRDB Bank Foundation imetenga Euro milioni 24 sawa na Shilingi bilioni 67 kwa ajili ya programu hii zitakazotolewa ndani ya miaka mitatu ya ushirikiano wetu na SUGECO ili kuwaandaa vijana mahiri watakaoajiria au kujiajiri kwenye sekta ya kilimo,” amesema Tully.


Tangu kuanzishwa kwake, SUGECO huwapeleka nje ya nchi wahitimu wa SUA hasa katika mataifa ya Ulaya, Amerika na Asia ambako hujifunza namna nzuri ya kufanya kilimo chenye tija lakini mchakato huo huhitaji fedha za awali kumwezesha mhitimu husika kujiandaa ipasavyo.


Kwa mwaka huu wa kwanza, Tully amesema wanatarajia kuwawezesha zaidi ya wahitimu 2,500 kwa kati ya dola 3,500 za Marekani (shilingi milioni 8.7) mpaka dola 4,500 (shilingi milioni 11.29) zinazotosha kwa mahitaji yao yanayojumuisha gharama za pasi ya kusafiria, visa pamoja na fedha ya kujikimu kabla ya kuanza kulipwa huko waendako.


“Mpango wa uwezeshaji baada ya mafunzo pia umeshaandaliwa kwa kushirikiana na SUGECO pamoja na USAID kwa kutenga maeneo maalum ya kuwekeza katika kilimo cha kisasa, na chenye tija zaidi. Taasisi yetu imejipanga kikamilifu pia katika hatua hiyo ya pili ya uwezeshaji kwa kutoa mitaji wezeshi, pamoja kuwapa mafunzo ya ujasirimali,” amesisitiza Tully.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SUGECO, Ndugu Revocatus Kimario amesema ushirikiano na Taasisi ya CRDB Bank Foundation utaongeza idadi ya wanufaika kwa kiasi kikubwa kwani mwaka jana waliweza kuwapeleka vijana 500 tu kupata mafunzo hayo kwa vitendo nje ya nchi ili kupata elimu na kujengewa uwezo zaidi katika kilimo, fani ambazo wamezisomea.


“Ushirikiano huu, tunaamini utakuwa na tija kubwa kwani ili ufanye biashara endelevu ni muhimu kuwekeza kwa watu unaowahudumia. Mkataba huu ni kati ya uwekezaji mkubwa kwa Benki ya CRDB kwani si wahitimu peke yao watakaonufaika bali wafanyakazi wao, familia hata ndugu, jamaa na marafiki zao,” amesema Kimario.
Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya SUGECO naye, Dkt Anna Temu alikumbusha namna walivyouanzisha ushirika huo ambao mpaka sasa umewaneemesha maelfu ya wahitimu wa SUA kwa kuwaongezea maarifa juu elimu waliyoipata darasani.

“Kwa kuwa sisi tunawahudumia zaidi vijana na wanawake, tuliona CRDB Bank Foundation wenye Program ya Imbeju ni wabia muhimu wa kufikisha malengo yetu kwa jamii,” amesema Dkt Anna.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com