WAANDISHI wa habari wametakiwa kupaza sauti zao kuwatetea wananchi kupitia vyombo vya habari kwa maslahi ya kukuza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza ambao utasaidia kuleta maendeleo ya haraka kwa taifa.
Uhuru huo unaweza kupatikana endapo kutakuwa na sheria rafiki za habari sambamba na waandishi wenyewe kufanya kazi kwa kufuata maadili ya tasnia yao na kuendeleza jukumu la huleta maendeleo kutokana na kuwa kiungo cha kupaza sauti kwa wasio na sauti .
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) Dkt Mzuri Issa Ali wakati wa mafunzo ya siku moja ya kupitia Mikataba ya kikanda na ya Kimataifa na kujadili mapungufu ya sheria zinazokwamisha uhuru wa habari Zanzibar.
Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo yaliyowakutanisha watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo , Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar, Tume ya Utangazaji na waandishi wa habari ni kukumbushana umuhimu wa kuangalia ni kwa kiasi gani kama nchi imeweza kuzingatia mikataba hiyo ili kupata sheria na sera bora zitakazo simamia masuala ya haki ya kupata habari na kutoa maoni na kukuza demokrasia nchini.
Aidha amebainisha kuwa pamoja na kuridhia Mikataba ya bado sauti za wananchi hazipewi kipau mbele kusikika katika vyombo vya habari ukilinganisha na sauti za viongozi jambo ambalo linawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights (UDHR), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (The International Covenant on Civil and Political Rights (ICCPR) na Mkataba wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa Umoja wa Afrika (African Charter on Human and Peoples Rights - ACHPR)
“ Nchi nyingi za Afrika zimeweza kupiga hatua za kimaendeleo kwa kuvitumia vyema vyombo vya habari kwa uhuru na kupelekea kuinua uchumi wa nchi ambapo ni pamoja na Ghana, Afrika ya kusini na Mozambique.
Mapema akiwasilisha mada kuhusiana na “Mapungufu ya Sheria za habari” Bibi Hawra Shamte ambae ni mwandishi wa habari mkongwe amesema ingawa kuna sheria zinazosimamia sekta ya habari bado zinaonekana kiuhalisia hazifanyi kazi ipasavyo kwa kulinda usalama wa waandishi wa habari na wananchi hivyo zinahitaji kufanyiwa marekebisho.
“Baadhi ya sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu No. 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria No. 8 ya mwaka 1997 na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar No. 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho na sheria No 1 ya 2010”, alieleza muwasilishaji huyo.
Wakichangia katika mafunzo hayo, miongoni mwa waandishi wahabari wamesema wamaekuwa wakikutana na vikwazo mbalimbali katika kufanikisha majukumu yao, hali inayosababisha kukosa uhuru na kutowajibika ipasavyo.
Mafunzo hayo yametolewa na TAMWA-ZNZ kwa watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo,Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar, Tume ya Utangazaji na waandishi wa habari yenye lengo la kuonesha umuhimu wa kuzingatia mikataba ya kikanda na ya kimataifa ili kuwa na sheria na sera bora zitakazo simamia masuala ya haki ya kupata habari na kutoa maoni kwa uhuru.