Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAWA YAWEKA KAMBI RUFIJI, ELIMU YA KUEPUKA MADHARA YA MAMBA NA VIBOKO YATOLEWA

 



Na. Beatus Maganja

Timu ya Maofisa uelimishaji kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imeweka kambi maalumu wilayani Rufiji yenye lengo la kutoa elimu ya namna ya kuepuka madhara yatokanayo na mamba na viboko kwa wananchi walioathiriwa na mafuriko wilayani humo.

Hayo yamesemwa leo na Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wilayani humo.

"TAWA tumeweka Kambi katika wilaya ya Rufiji kufuatia mafuriko yaliyojitokeza katika wilaya hii yaliyoathiri watanzania wenzetu" amesema

"Jambo lililotuleta hapa, kwanza ni kutoa pole kwa watanzania wenzetu ambao wamekumbwa na mafuriko haya, lakini pia tumekuja mahsusi kwa ajili  ya kutoa elimu ya namna  wananchi hawa wanaweza kuchukua tahadhari kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu kama vile mamba na viboko" ameongeza Maganja

Afisa uelimishaji kutoka TAWA Kanda ya Kusini Mashariki Jimmy Mshana amesema TAWA ilianza kutoa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali wilayani humo ikiwemo Kata ya chemchem na vitongoji vyake vyote na leo Aprili 15, 2024 elimu hiyo imeendelea kutolewa katika Kata ya mgomba na vijiji vyake vyote na kukiri kupata mwitikio mzuri kutoka kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha mgomba kusini Kassim Ally Mtumbei ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa elimu ya kujikinga na madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu waliyoipata kutoka kwa maofisa wa TAWA walioweka kambi wilayani humo.

 Imeelezwa kuwa mafuriko katika wilaya hiyo mbali na kuharibu makazi ya watu na mali zao,  yameambatana na athari mbalimbali ikiwemo ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko ambao wametoka kwenye maeneo yao ya asili na kusogea karibu na makazi ya watu kwa kusafirishwa na mikondo ya maji.

Ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao, TAWA imepeleka vikosi vya doria kwa ajili ya kuwadhibiti na kutoa elimu kwa jamii ya kuchukua tahadhari kuepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao, na hii ni katika kuonesha namna ambavyo TAWA inavyothamini na kujali maisha ya binadamu



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com