Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mkoa wa Mbeya Bi. Anna Mwambene amewaasa wafanyabiashara wa Mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kutumia Baraza la Ushindani (FCT) katika kutatua changamoto za kibiashara zinazotolewa maamuzi na Mamlaka za Udhibiti au Tume ya Ushindani zilizoanishwa katika Sheria ya Ushindani, 2003 kustawisha ushindani wa haki na kumlinda mlaji katika Soko.
Bi. Mwambene ameyasema hayo alipokuwa akifungua Semina ya elimu kwa Wadau Baraza la Ushindani (FCT) iliyofanyika Aprili 4 2024 jijini Mbeya.
Akiwa anatoa mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Uchumi katika Baraza hilo Bw. Kulwa Msogoti alieleza kuwa Baraza la Ushindani ni Taasisi ilivyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoanzishwa chini ya kifungu cha 83(1) cha Sheria ya Ushindani Namba 8 ya Mwaka 2003.
Aidha, alieleza kuwa Baraza hilo lilianzishwa kwa dhumuni la Kukuza na kulinda ushindani wenye tija katika Soko na kuzuia mwenendo na tabia potofu katika Soko la Tanzania ili Kuongeza ufanisi na uzalishaji, usambazaji wa huduma na bidhaa, Kukuza ubunifu, Kuwezesha matumizi ya rasilimali yenye ufanisi na Kumlinda mlaji.
Pia, aliendelea kueleza kuwa dhumuni hilo linatekelezwa kwa kushughulikia migogoro ya Wafanyabiashara, Wawekezaji, Watoa huduma na Walaji ikiwemo jamii inayohusu ushindani wa kibiashara na udhibiti wa Soko kwa njia ya kupokea, kusikiliza na kuamua kesi za rufaa zinazopokelewa na Baraza hilo.
Akieleza zaidi Bw. Msogoti amesema Baraza hilo hupokea, kusikiliza na kuamua kesi za rufaa zinazotokana na maamuzi yaliyotolewa Tume ya Ushindani-FCC, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA).
Nyingine ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano (TCRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Nishati ya Petroli (PURA).
Aidha, aliendelea kufafanua zaidi kuwa toka kuanza usikilizaji wa kesi, kuanzia 2007 hadi Machi, 2024 Baraza limesajili jumla ya mashauri 442 ambapo kati ya hayo mashauri 429 sawa na asilimia 97.1% yameshasikilizwa na kutolewa maamuzi na mashauri 13 yaliyobaki yapo kwenye hatua mbalimbali za usikilizwaji.
Aidha, Bw. Msogoti alibainisha kuwa Matokeo ya maamuzi ya mashauri hayo yameongeza uwajibikaji kwa Wadau wote katika Soko na kuchochea makampuni kuongeza umakini katika kufuata Sheria za nchi, kuongezeka kwa uwazi na ushindani wa bei katika biashara mbalimbali nchini, uwajibikaji kwenye ushindani katika sekta ya biashara na udhibiti wa Soko.
Naye Afisa Sheria Mkuu wa Baraza hilo, Bi. Hafsa Said alifafanua kuwa Mtu binafsi, Kampuni ya biashara au Taasisi anaruhusiwa kuwasilisha maombi ya rufaa na lazima ithibitishe kuwa, uamuzi unaoombewa rufaa lazima uwe umefanywa na moja ya Mamlaka za Udhibiti zilizotajwa hapo awali au Tume ya Ushindani.
Vilevile alieleza kuwa muomba rufaa lazima awe miongoni mwa Wadaawa (Party) wa mgogoro ulipokuwa kwenye Mamlaka ya Udhibiti au Tume ya Ushindani.
Social Plugin