Picha ikionesha moja ya chungu cha maua kilichowekwa kando ya barabara kikiwa kimewekwa uchafu ambao haukujulikana umewekwa na nani.
Na Dotto Kwilasa,DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma limedhamiria kushirikiana kwa ukaribu na watu wa usalama barabarani, polisi jamii,wasimamizi wa mandhari na watu wa sheria ndogo ndogo za uhifadhi katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira unaotokana na utupaji taka maeneo ya wazi na mengineyo.
Hatua hii ni kutokana na kuwepo kwa tabia iliyoibuka ya kutupa taka kwenye maeneo ya wazi hususani kwenye vyungu vya maua vilivyowekwa kwenye barabara kuu ya Nyerere (Kuu street ) kwa ajili ya kupendezesha Mandhari ya jiji la Dodoma kugeuzwa kuwa sehemu ya kuhifadhia uchafu .
Vyungu hivyo ambavyo vimezungushwa na kusambazwa kwenye Barabara hiyo vimeonekana kutotunzwa wala kuthaminiwa kutokana na hali hiyo ya kuenezwa uchafu kwa siri siku hadi siku.
Akizungumza jijini hapa,Afisa Mazingira wa jiji la Dodoma Dickson Kimaro amesema suala la uchafu linatia kichefuchefu kwani linaweza kusababisha magonjwa na kurudisha nyuma maendeleo na kuwataka wanaotupa taka bila utaratibu kuacha mara moja .
Amesema kutokana na hali hiyo wamekuwa tukikamata wanaofanya uchafu na kuwapiga faini ya shilingi 300000 na kwa wanaobainika kuvigonga vyungu hivyo wanalipa faini ya shilingi 300000 na kutengeneza na kurudisha mmea au ua kama lilivyokuwa .
Kimaro amesema lengo la kuwepo kwa vyungu hivyo ni kupendezesha jiji la Dodoma liwe jiji la kijani (Green city) lakini imetokea kwa baadhi ya wananchi kuvigonga usiku wakiwa wamelewa na wengine kutupa taka ndani ya vyungu hivyo jambo ambalo halifai.
"Hii tabia ni hatari ambayo hufanywa na wananchi wanaoishi au kufanya shughuli zao maeneo ya barabara wakiwemo madereva wa daladala, waendesha bajaji , pikipiki na watembea kwa miguu,lazima tujue kutunza Mazingira ili yatutunze ,tunapotupa chupa ya plastiki ndani ya mmea tambua unakwenda kuuua kwani chupa au uchafu unaoutupa ina kemikali,"amesema
Sambamba na hayo ametoa wito kwa baadhi ya wafanyabishara hususani wanaokaanga Chipsi na mishikaka kuacha kutupa majivu ya moto kwenye vyombo vya kuhifadhia uchafu kwani wamekuwa wakisasabisha vyombo hivyo kuungua kutokana na material yake kuwa ya plastiki.
Aidha amesema kutokana na tatizo hilo Serikali kwa kushirikiana na wadau wapo kwenye mpango wa kuhakikisha wanasambaza vyombo vya kuhifadhia uchafu vya chuma ili hata vikimwagiwa moto viweze kuhimili.
Mwenyemiti wa Mtaa wa Tofiki Alnoor Visram amezungumzia hali hiyo kuwa yeye kwa nafasi yake amekuwa akihimiza wananchi wake kuzingatia suala la usafi lakini imekuwa ni Changamoto kubwa .
"Ni kweli vyungu hivyo vimegeuzwa vibebeo vya uchafu na hiyo yote ni kutokana na eneo au Mtaa wake kuwepo katikati ya mji ambao una watu wenye tabia tofauti na kushindwa kutii kanuni za usafi,kwakweli ni aibu kubwa ukizingatia hii ndio barabara kubwa hapa mjini na tukiwa tumezungukwa na ofisi kubwa bila kusahau ofisi kuu ya CCM,niombe kuwepo na utaratibu kwa watu kama hao kukamatwa na kuadhibiwa tena adhabu kali, "amesisitiza na kuongeza;
Sisi kama viongozi hasa wa Mtaa hatujapewa rugu la kuwakamata moja kwa moja na kuwawajibisha wale wote wanaoonekana kutupa taka hizo lakini tungepewa nafasi hii tunaimani mazingira yangekuwa safe,nitoe wito kwa Wananchi wa jiji la Dodoma kuheshimu sheria za utunzaji wa mazingira na kila mtu au Wananchi awe askari wa manzingira ili mwenzako asiweze kutupa uchafu hovyo, " amesema
Kutokana na hayo ameiomba Serikali kuingilia kati suala hilo kwa kutoa kalipio kali kwa wote wataobainika kutupa uchafu hovyo ikiwa ni pamoja na kuwajibisha kisheria.
Naye Jafary Mnyawi mkazi wa Dodoma Kata ya Miyuji amesema Licha ya Dodoma kuwa jiji lakini ukweli ni kwamba Dodoma ni chafu tofauti na majiji mengine hapa nchini.
"Nitoe ushauri kwa Serikali kuwepo na utaribu na sheria za kuwawajibisha wachafuzi wa mazingira wote, mtu akitupa taka akamatwe kama wanavyofanya katika mikoa ya Moshi na arusha ,Dodoma ni jiji hivyo ni lazima jiji liwe safi na kupendeza, " Amesema mkazi huyo Mnyawi
Social Plugin