Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, akizungumza wakati akiongoza maadhimisho ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yaliyofanyika Leo Aprili 15,2024 jijini Dodoma.
Makamu Mkuu wa Chuo cha UDOM Prof. Lughano Kusiluka akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yaliyofanyika Leo Aprili 15,2024 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani), wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yaliyofanyika Leo Aprili 15,2024 jijini Dodoma.
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amewasisitiza wanafunzi wanaohitimu masomo ya Sheria nchini kuwa na utamaduni wa kujisomea kwani kwasasa dunia inapitia mabadiliko makubwa ya matumizi ya Teknolojia kwenye utendaji wa kazi.
Jaji Mkuu ameyasema hayo leo Aprili 15,2024 Jijini Dodoma wakati akiongoza maadhimisho ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambapo yameongozwa na kauli mbiu isemayo “Uimarishwaji wa kliniki za sheria vyuo vikuu katika kukuza na kupanua wigo wa upatikanaji wa haki Tanzania”.
“Maarifa katika Karne ya 21 huletewi, unatafuta na unatafuta kwa kusoma bahati nzuri tuna mifumo mizuri ya Teknolojia ambayo inatuwezesha kusoma na Mwalimu Nyerere alisema wenzetu wanapotembea sisi tunapaswa kukimbia,”amesema.
Amesema hivyo katika zama hizi za teknolojia wanapaswa kukimbia ili kwenda sawa na wenzao kwani kasi ya mabadiriko ni kubwa sana.
Aidha amesema kwasasa kuna changamoto kubwa ya mrundikano wa mawakili katika maeneo ya mjini hivyo amewaomba wanafunzi hao pindi watakapohitimu masomo yao kusambaa katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Vijijini ili kuweza kuwasaidia wananchi wanaopitia changamoto za kisheria.
“Mnapokutana na wananchi katika kutoa msaada wa Kisheria moja ya majukumu yenu ni kuhakikisha mnafahamu changamoto za kisheria ambazo zinawakabiri wananchi wa kawaida, kuna watu wapo Tanzania lakini hawajui uhalisia wa changamoto zinazo wakabiri wananchi wa kwaida,”amesema.
Pia ameongeza kuwa hakuna uwekezaji mkubwa kama uwekezaji wa maarifa kwani Karne hii ya 21 inahitaji zaidi maarifa ili kuweza kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha UDOM Prof. Lughano Kusiluka ameiomba Mahakama kuwa na matawi ya vyuo vya sheria kila kanda ili kuweza kuwasaidia wanafunzi wanaotaka kusoma sheria kubakia katika maeneo yao kuliko kusafiri kufuata vyuo hivyo sehemu za mbali.
“Mimi nashauri ila mtaangalia kama litakuwa ni jambo jema kwakuwa tuna Majaji wengi kwenye kanda na hao ndiyo wakuwafundisha hawa kwenye mafunzo kwa vitendo, kwakuwa tuna TEHAMA ambayo inaweza ikawasaidia watu kusoma na vitendo nadhani ingekuwa ni vizuri Mahakama ikafikiria kuwa na matawi ya shule za Sheria angalau katika kila kanda ili vijana hawa waweze kusoma huko,”amesema.
Amesema wamekuwa wakishirikiana vyema na Wizara ya Katiba na Sheria na wadau wengine kama njia ya kuweza kuwajengea uwezo na ufanisi mkubwa vijana wanahitimu masomo yao ya Sheria.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa mwaka huu yanaadhimishwa kwa mara ya Tatu rangu yaasisiwe.
Social Plugin