NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), wameiomba Serikali katika mchakato wa uandaaji wa bajeti kuwawekea wananchi vipaumbele ambavyo vitawasaidia kuwakwamua katika masuala ya uchumi, kilimo pamoja na elimu jambo ambalo litachangia kuishi kwa usawa.
Kauli hiyo imetolewa leo April 03,2024, katika semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), ambazo zimekuwa zikifanyika kila Jumatano katika Ofisi za TGNP Mtandao, Mabibo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika sehemu hizo, Mwanaharakati wa jinsia ngazi ya jamii, Kata ya Mabibo Bw.Venance Mbena amesema kuwa wanatarajia kuona serikali ikionesha bajeti inajielekeza kwenye suala gani.
Aidha amesema mambo wanayojadili wanatamani yafike katika mitaa yao ,wilaya hadi serikali kuu kwani wao kama wanaharakati ndio wanaoibua changamoto kwenye jamii na kupigania waliopo mijini na vijijini.
Kwa Upande wake, Mdau wa semina za Jinsia na Maendeleo, Bi.Nanteka Maufi ameeleza kuwa wananchi hawapati fursa ya kushiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kabla ya bajeti kwenda kujadiliwa bungeni.
"Sisi muwakilishi wetu ni diwani,lakini sisi kama wananchi tunajikuta ni waoga wa kuhudhuria mikutano,nawashauri wananchi kuhudhuria mikutano kwa sababu hata katiba inatulinda kutoa maoni"Bi.Nanteka ameeleza.
Naye Mwanaharakati wa Jinsia kata ya Makurumla Wilaya ya Ubungo Bi.Rhoda Abdul ametoa hamasa kwa wananchi kufatilia bunge la bajeti,kuona vitu gani vipya ambavyo vimewekwa katika bajeti ili kutoa kero zao pale wanapoona changamoto zinazowakabili hazijatatuliwa.
Social Plugin