WATETEZI KABILIANENI NA MBINU CHAFU ZA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU - OLENGURUMWA


Mratibu wa kitaifa wa Shirika la watetezi wa haki za binadamu Onesmo Olengurumwa akifungua mafunzo hayo

Na Christina Cosmas, Morogoro

WATETEZI wa haki za binadamu wamesisitizwa kuhakikisha wanapata elimu za mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto za mbinu chafu za mikakati ya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo wizi wa kimtandao.

Mratibu wa kitaifa wa kutoka shirika la watetezi wa haki za binadamu (THRDC) Onesmo Olengurumwa amesema hayo wakati wakitoa mafunzo ya watetezi wa haki za binadamu kutoka maeneo ya nje ya miji kwenye kanda tatu nchini kupitia mtandao wa haki za binadamu.

“Zipo mbinu mpya mbalimbali ambazo wahalifu wanazitumia kwa njia ya mtandao za kukiuka haki za binadamu, mtetezi nae lazima afahamu ni namna gani anaweza kushughulikia na kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanyika ili kuendana na kazi ya mhalifu au mkiukaji wa haki za binadamu anayokwenda nayo” anasema Olengurumwa.

Aidha anasema watoto wamekuwa wakibakwa na watu mbalimbali wakiwemo watu wao wa karibu au viongozi wa dini kwa njia na mbinu mbalimbali ikiwemo kuwalaghai kwa kuwanunulia zawadi na mengine ambayo mtetezi wa haki za binadamu akijua itamsaidia kufuatilia masuala hayo ya ukiukwaji na kuweza kuwa mtetezi mzuri.

Naye Mwanasheria kutoka kituo cha wasaidizi wa kisheria Morogoro (MPLC) Rachel Siwiti alisema wakiwa watetezi wa haki za binadamu kwa wanawake na Watoto tayari wameshafikia asilimia 70 ya kutoa elimu kwa jamii licha ya kwamba bado haina mwamko wa kupokea elimu na kuondoa changamoto hizo.

Siwiti aliishukuru THRDC kwa kuendelea kuwapa mafunzo yatakayowaimarisha kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo wanawake kuonewa kwa kutopata haki zao kama vile mirathi na mkoa kuwa na ndoa nyingi za utotoni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم