Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KAIRUKI, DKT. ABBASI WAYAJENGA NA WADAU WA UTALII


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewapongeza wadau wa utalii nchini kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya sekta hiyo katika kipindi hiki ambapo utalii umekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia kwenye mapato ya fedha za kigeni.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo Aprili 6, 2024 mjini Arusha akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi kwenye mkutano wa pamoja baina ya Wizara na wadau wa sekta ya utalii ambao ni Chama cha Waongoza Utalii, Wakala wa Usafirishaji Utalii, Vyama vya Wamiliki wa Huduma za Malazi na Vyama vya Wabeba Mizigo kujadili masuala mbalimbali ili kuboresha sekta hiyo.

Aidha, amesema wadau wa utalii wana mchango mkubwa katika uchumi wa taifa ambapo amefafanua kuwa sekta hiyo inachangia takribani asilimia zaidi ya 25 ya mapato ya fedha za kigeni na kutoa fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine muhimu.

Katika mkutano huo Waziri Kairuki amemtaka Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB) ambaye ameteuliwa hivi karibuni bwana Ephraim Mafuru kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii nchini ili kuendelea kuvitangaza vivutio vya utalii duniani.

Ametoa wito kwa waongoza watalii kuwa wazalendo kwa kuwa wao ndiyo mabalozi wa taifa huku akisisitiza kuwa wageni hukaa nao kwa muda mwingi hivyo ni muhimu kutoa taarifa sahihi.

Akiongea katika kikao hicho, Muongoza utalii, Hope Tumaini ambaye amekuwa kwa zaidi ya miaka 15 ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya huku akiomba Serikali kutoa mafunzo maalum kwa waongoza watalii hususan wanawake.

Mhe. Waziri amesema kuanzia mwakani Serikali itatoa mafunzo ya utalii kuanzia kwenye ngazi ya Sekondari ambapo wadau wa utalii pia watahusishwa katika maandalizi ya mitaala ya utalii ili mafunzo hayo yawe na tija.

Katika mkutano huo baadhi ya mambo ambayo yamejadiliwa na kupatiwa ufumbuzi wakati mengine yakiendelea kufanyiwa kazi.

Baadhi ya mambo ambayo yamepatiwa ufumbuzi leo ni pamoja na kupunguza ada ya leseni ya waongoza Utalii iliyokuwa USD 50 kila mwaka ambapo sasa itakuwa laki moja kila baada ya miaka 3 ada hiyo itaanza Januari 2025 pia malipo ya ada ya leseni hiyo ya waongoza watalii ya dola za kimarekani 50 sasa itaanza kulipwa kwa shilingi za kitanzania kuanzia Julai mwaka huu.

Aidha, Mhe. Kairuki amefuta viingilio kwa waongoza watalii katika mageti ya hifadhi kwa waliolipia leseni zao za usajili.

Wadau hao wa Sekta ya Utalii wametumia mkutano huo na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mabadiliko chanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake, huku wakisifu kasi ya sasa ya utendaji wa Wizara.

Awali akimkaribisha Waziri Kairuki katika mkutano huo Dkt. Abbasi amesisitiza kuwa katika kipindi hiki Serikali itakuwa karibu na wadau kwenye kila hatua ili kuhakikisha sekta inasonga mbele kwa maslahi ya wadau na taifa kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com