Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA AZINDUA DIRISHA LA MAKISATU


Na Dotto Kwilasa, DODOMA

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefungua dirisha la usajili wa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaani (MAKISATU) zitakazopelekwa kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2024 huku Mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa. 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amezungumza hayo leo Aprili 9,2024 jijini hapa alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho hayo. 

Aidha, amesema katika kilele cha Maadhimisho hayo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

" Mwaka huu Wizara imeanza utaratibu mpya ambapo tutakuwa na Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu hii ni matokeo ya kuunganisha yaliyokuwa Maadhimisho ya Kitaifa ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama MAKISATU," Amesema 

Na kuongeza, "Maonesho ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yaliyokuwa yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET); na Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyokuwa yanaratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), " Amesema 

Ameeleza kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongeza hamasa ya kukuza elimu, ujuzi, na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kusaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii pamoja na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla. 

Amesema Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yatazileta pamoja Taasisi, Mashirika, Wadau wa Maendeleo, Asasi, Watunga Sera, Wabunifu/wagunduzi, na Wadau wengine mbalimbali kwa ajili ya mijadala, na kushuhudia tafiti, bunifu na teknolojia zinazozalishwa nchini.  

"Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa wabunifu na watafiti nchini kuonana na wawekezaji wanaoweza kuchangia kwa namna mbalimbali katika kuendeleza na kubiasharisha matokeo ya tafiti na bunifu zao, " Amesema Prof 

Hata hivyo amebainisha kuwa,Maadhimisho ya mwaka 2024 yatafanyika Mkoani Tanga kuanzia tarehe 25 hadi 31 Mei 2024 katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Popatlal. 

"Kaulimbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Tanzania kwa mwaka 2024 ni Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi Shindani ambayo inachagiza umuhimu wa elimu, ujuzi na ubunifu na teknolojia katika maendeleo ya kiuchumi," Amesema Prof Mkenda. 

Na kuongeza kusema "Serikali imeendelea kuwekeza katika kuendeleza na kubisharisha bunifu na teknolojia zinazobuniwa hapa nchini. Katika kipindi cha mwaka 2019 na 2023 zaidi ya bunifu 2000 zimetambuliwa na 283 kati ya hizo zinaendelezwa," Amesema

Aidha amesema, bunifu 42 zimeweza kufikia hatua ya kubiasharishwa na ziko sokoni. Bunifu hizo zinatumika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta za kilimo, maji, nishati, afya na elimu. 

Pia Maadhimisho ya mwaka 2024 yatahusisha maonesho ya bidhaa, bunifu na teknolojia mbalimbali,Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu 

(MAKISATU)Mashindano ya ujuzi `Skills Competition` kwa wanafunzi wa vyuo vya Ufundi na Ufundi Stadi,Mikutano na Midahalo kuhusu elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu pamoja Mafunzo kwa wabunifu. 

Amesema Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yatatanguliwa na matukio katika ngazi za mikoa na halmashauri ikiwemo maonesho ya ubunifu na teknolojia, mikutano na midahalo chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Programu ya FUNGUO-UNDP, Ofisi za Makatibu Tawala Mikoa na wadau wengine. 

"Mwaka huu tunatarajia kuwa na washiriki kutoka taasisi za umma na binafsi zipatazo 339 watakaojumuisha Vyuo Vya Elimu ya Juu na Taasisi mbalimbali kutoka nje ya nchi,hivyo, ninaomba kutumia fursa hii kuzialika taasisi za umma na binafsi, mashirika, wizara na wadau wengine ndani na nje ya nchi, kushiriki katika Maadhimisho haya, " amesema 

Pamoja na hayo ameongeza, "Mashindano haya yatahusisha wabunifu kutoka Vyuo Vya Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo, Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Shule za Msingi, Shule za Sekondari na wabunifu kutoka Mfumo usio rasmi ambapo Washindi 10 kwa kila kundi watashiriki katika maadhimisho ya ngazi ya kitaifa. 

Aidha, washindi wa jumla wataingia katika mpango wa Serikali wa uendelezaji na ubiasharishaji wa bunifu zao, " Amesema.  

Pia amebainisha kuwa Mashindado ya ujuzi yatafanyika katika ngazi ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika fani mbalimbali Ambapo Washindi watano kwa kila fani watashiriki katika maadhimisho ya wiki ya kitaifa huku Washindi wa jumla watatangazwa na kupata zawadi mbalimbali katika siku ya kilele cha maadhimisho hayo ikiwemo kushiriki katika mashindano ya ujuzi ya kidunia.  




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com