Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza wakati wa kuaga miili ya wanafunzi watatu waliofariki dunia kwa kukosa hewa safi kwenye kihenge cha mahindi
NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL& HUHESO FM
Wanafunzi watatu (3) wa shule ya sekondari John Paul wa pili iliyopo Mtaa wa Mbulu Kata ya Mhongolo Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wamefariki dunia kwa kukosa hewa baada ya kuingia kwenye kihenge cha kuhifadhia mahindi kwa lengo la kutoa mahindi hayo kwa ajili ya chakula.
Akizungumza leo wakati ibada ya kuaga miili ya Wanafunzi hao iliyofanyika kwenye viwanja vya Jimbo Katoliki la Kahama Mjini Wilayani Kahama
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa vijana watatu wanaosoma kidato cha tatu katika shule ya Sekondari John Paul wa pili walikuwa wameingia kwenye Kihenge cha kutolea mahindi kwa ajili ya chakula na hawakujua madhara ya Kihenge hicho na hewa haitoshi hali ambayo ilisababisha kifo chao.
Akitoa salamu za Rambirambi kwa wafiwa, mdhibiti wa Ubora wa Elimu wa Kanda Edith Mwijage amesema kuwa amesikitishwa na tukio la vijana hao na kutumia nafasi hiyo kuwaomba wazazi kuwa na subira wakati wakati wa kipindi hiki kigumu ambapo wamepoteza wapendwa wao.
Naye Japhet Daud Mdadila akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake amesema kuwa kwao kama wazazi pamoja na kanisa na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla huo ni msiba mzito na wameupokea kwa masikitiko makubwa.
"Sisi wanadamu tumezaliwa na mwanamke siku zetu zinahesabika, Viongozi wa Dini wametuhubilia hata tungelaumu kiasi gani na hata tungesema changamoto nyingi sana nasi hili tumepewa ni somo kwetu",amesema.
Waliofariki katika tukio hilo ni pamoja na Jonathan Daud Mdadila (17) Mkazi wa Nzega, Ibrahim Juma Said (17) Mkazi wa Mwanza pamoja na Paul Emmanuel John (18) Mkazi wa Kahama.
Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Kenedy Mgani amesema tkio hilo lilitokea Mei mosi mwaka huu na kwamba walifariki dunia kwa kukosa hewa safi baada ya kuingia kwenye kihenge cha kuhifadhia Mahindi.