Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akitoa hotuba wakati wa Kongamano la Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) lililofanyika leo Jumanne Mei 21,2024 katika ukumbi wa Maktaba Chuo Kikuu cha Dar es salaam - Picha na Kadama Malunde
*Sheria huduma za habari kufanyiwa Marekebisho kulinda uhuru wa habari
Na Marco Maduhu,Dar es salaam
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) katika nyanja mbalimbali, ikiwamo na kufanya Marekebisho ya sheria za huduma za habari ili kulinda uhuru wa habari.
Amebainisha hayo leo Mei 21,2024 wakati akitoa hotuba alipokuwa Mgeni Ramsi kwenye Kongamano (JUMIKITA) na Miaka Mitatu ya Rais Samia Madarakani,lililoenda Sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari ambayo kitaifa yalifanyika Mei 3 Jijini Dodoma.
Amesema anaipongeza Jumuiya hiyo kwa kuwaunganisha Waandishi wa habari za Mitandaoni kuwa wamoja na kuwasihi wale ambao hawajajiunga na JUMIKITA wajiunge haraka, ili wawe kitu kimoja na kupatikana kwa urahisi.
"Serikali ipo tayari kushirikiana na JUMIKITA,na wale ambao hawajajiunga waenda ili muwe kitu kimoja,na sisi tunapowahitaji tujue tunawapata wapi na kwa urahisi. Waandishi wa habari mtandaoni mnafanya kazi nzuri, nyie endeleeni kutimiza majukumu yenu, tunawahakikishia kuwa serikali hii iko pamoja nanyi, pia kila mmoja ajikite kwenye eneo analoweza kubobea, endeleeni kufanya kazi ya kutangaza nchi", amesema Majaliwa.
Amesema katika kuendelea kutoa Uhuru wa habari na kuulinda, Serikali itaendelea kufanya mapitio na marekebisho ya Sheria za huduma za habari ambazo siyo rafiki.
Aidha, amesema Serikali inatambua, kuthamini na kuheshimu mchango mkubwa wa Mitandao ya Kijamii na hata nchi za jirani ikiwamo Kenya zimekuwa zikiifuatilia nchi ya Tanzania kila kukicha kupitia mitandao ya kijamii kutokana na kazi kubwa ambayo inafanywa na waandishi wa habari kwa kuitangaza nchi yao.
"Sekta ya Mitandao ya Kijamii imesaidia kutengeneza ajira kwa vijana. Nyinyi ni watu muhimu katika nchi, na serikali inawatambua mchango wenu, tunathamini mchango wenu na tunaheshimu mchango wenu na tunaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya kazi na nyinyi",amesema Mhe. Majaliwa.
"Wamiliki wa mitandao ya kijamii mnafanya kazi kubwa na nzuri, kupitia mitandao ya kijami tumefanikiwa kutoa taarifa mbalimbali. Nyie endeleeni kutimiza majukumu yenu, tunawahakikishia kuwa serikali hii iko pamoja nanyi, kila mmoja ajikite kwenye eneo analoweza kubobea, endeleeni kufanya kazi ya kutangaza nchi yetu.
Nchi mbalimbali zimekuwa zikiingia kwenye mitandao ya kijamii ya Tanzania kusoma habari mbalimbali,hongereni sana",ameongeza.
Amewasihi waandishi wa habari kuendelea kuitangaza Serikali kwa mazuri ambayo imeyafanya,ikiwamo na Miradi ya Kimkakati ambayo inaendelea kutekelezwa, pamoja na kuandika habari ambazo hazina viashiria ya uvunjifu wa Amani.
Katika hatua nyingine amesema kutokana na Mitandao ya Kijamii kuwa na Mchango mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana, kwamba Rais Samia ameweka Mkakati wa kujenga Jengo kubwa la TEHAMA Jijini Dodoma,ambapo vijana wote wenye ubunifu watapata nafasi ya kulitumia.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka waandishi wa habari kukemea aina zote za ubaguzi unaolenga kugawa taifa.
"Tukemee aina zote za kauli za ubaguzi, tusikubaliane na masuala ya ubaguzi, tusiruhusu wazungumzie ukanda, ukabila, wala utaifa hii ni nchi moja. Tusizungumzie masuala ya Uzanzibar na Utanzania, nyie mkikemea tutafika mahali pazuri, viongozi wetu, waasisi wa taifa hili walitujengea umoja na mshikamano",amesisitiza Waziri Mkuu.
Naye Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknlojia ya habari,Nape Nnauye, amesema ndani ya Miaka Mitatu ya Rais Samia wamepiga hatua kubwa katika Uhuru wa habari na hata kuongoza kwa nchi za Afrika Mashariki.
Amesema watakaa pia na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzanja (TCRA) kufanya Mapitio ya Sheria na kanuni ambazo zilikazwa sana ili zilegezwe, pamoja na mapitio ya Kodi na Tozo za kusajili blog na Online TV, kwamba kusiwepo na utozwaji wa Tozo kwanza, bali Mwandishi aanze kufanya kazi na ikifika kipindi flani ndipo aanze kulipa.
Mwenyekiti wa JUMIKITA Shaaban Matwebe, akizungumza kwenye Jukwaa hilo, amempongeza Rais Samia kwa kutoa uhuru wa habari ndani ya miaka yake Mitatu ya Utawala,huku akiomba Serikali kuwathamini pia Waandishi wa habari wa Mitandao ya kijamii, pamoja na kuwapatia Matangazo mbalimbali.
Amesema baadhi ya viongozi wenye Mamlaka wamekuwa hawawathamini Waandishi wa habari za Mitandaoni hasa wanapokuwa wakipiga Simu ili kubalance habari.
Pia, ameziomba Mamlaka mbalimbali za Serikali kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa Mitandaoni Kitaaluma, ili wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao wafanye kwa ufanisi mkubwa.
Naye Milard Ayo ameiomba Serikali kupitia TCRA kwamba kutokana na Mitandao ya Kijamii kutoa ajira kwa vijana wengi na wengine wanatoka Vyuoni hawana Mitaji, wapunguze Ada za kusajili Blog na Online TV sababu Sh. Laki Tano ni kubwa waipunguze pamoja na faini Sh.milioni 5, ili kutoa fursa ya kwa vijana kuendelea kujiajiri.