Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MACHA : RAIS SAMIA NI MSIKIVU, ATALIFANYIA KAZI SUALA LA KIKOKOTOO


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amewatoa hofu Watumishi wa Serikali juu ya suala la Kikokotoo, kwamba Rais Samia ni msikivu na atalifanyia kazi.

Amebainisha hayo leo Mei 1,2024 kwenye Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi dunia (MEIMOSI)mkoani Shinyanga yaliyofanyika Kata ya Kakola wilayani Kahama.

Amesema suala la Kikokotoo limesemwa vya kutosha kila Mahali hadi Bungeni, na kwamba ana imani Serikali imelisikia na italifanyia kazi kwa maslahi ya wafanyakazi.

"Tunaye Rais wetu msikivu na atalifanyia kazi suala la Kikokotoo," amesema Macha.
Aidha,amesema Rais Samia amekuwa akiboresha mara kwa mara Maslahi ya Watumishi wa Umma, pamoja na Mazingira mazuri ya kufanyia kazi ikiwamo na nyongeza ya mishahara.

Katika hatua nyingine amewataka Waajiri hasa wa Sekta binafsi kupelekwa Michango ya Watumishi wao kwenye Mifuko ya hifadhi ya jamii suala ambalo limekuwa likilalamikiwa na Watumishi mara kwa mara na hata kuleta Migogoro kwenye ulipwaji wa Mafao.


Amewasisitiza pia Waajiri wa Sekta binafsi kuzingatia Sheria za Ajira kwa Watumishi wao,pamoja na kuwapatia Mikataba mizuri isiyo Kandamizi,huku akiwasihi Watumishi nao wasikubali kupewa Mikataba Mibovu.
Amewahasa pia Watumishi wa Serikali hasa Walimu,Watumishi wa Afya na Kilimo kwamba wasijiingize kwenye Mikopo Kausha damu ambayo imekuwa ikiwadumaza Kimaendeleo.

Macha amewahidi Watumishi wa Serikali kwamba yale yote ambayo wamewasilisha kwenye Risala yao yanayogusa ngazi ya Kitaifa likiwamo pia suala la Kikokotoo na Vifurishi vya Bima ya Afya atayafikisha sehemu husika tena kwa maandishi.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Shinyanga Mathias Balele,akizungumza kwenye Maadhimisho hayo, amesema Kilimo kikubwa cha Wafanyakazi ni Kikokotoo.

Amesema tatizo la Kikokotoo ni kanuni na siyo Sheria,ambazo zinapaswa zaidi zile za zamani.

Naye Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Shinyanga Ramadhani Mpangala, akisoma Risala,amesema Changamoto kubwa ambayo inawakabili Wafanyakazi ni suala la Kikokotoo ambalo limekuwa Kaa la Moto kwa Wafanyakazi na kumuomba Rais Samia aliangalie upya.

Ametaja Changamoto zingine kuwa ni ucheleweshwaji Malipo ya Mafao kwa Wastaafu,Waajiri hasa Sekta binafsi kutopeleka Michango ya Watumishi katika Mifuko ya hifadhi ya jamii,pamoja na Waajiri kutoruhusu Watumishi wao kujifungua na vyama vya Wafanyakazi.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani Mwaka huu inasema" nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga dhidi ya hali ngumu ya Maisha."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com