SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA TIBA KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akitoa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini kwa mwaka 2023 kwa waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari Kamishna wa Kinga na Tiba Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) Dkt. Peter Mfisi akieleza jambo wakati wa Mkutano wa waandishi wa Habari.
Kamishna wa Kinga na Tiba Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) Dkt. Peter Mfisi akieleza jambo wakati wa Mkutano wa waandishi wa Habari.
Kamishna Jenerali  wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) Aretas Lyimo akifafanua jambo kuhusu  Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini kwa mwaka 2023 katika Ukumbi wa Habari Bungeni tarehe 16 Mei 2024 Jijini Dodoma.


Na Mwandishi wetu – Dodoma

Serikali imesema itaendelea kuboresha huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya ili kuhakikisha wanareejea katika hali zao za awali na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama  wakati akizungumza na waandishi kuhusu Taarifa  ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2023 tarehe 16 Mei 2024 katika Ukumbi wa Habari Bungeni Jijini Dodoma iliyoelezea mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya dawa hizo.

Mhe. Jenista alisema, mwaka 2023, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola vilifanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,965,340.52 za dawa za kulevya aina ya heroin, cocaine, methamphetamine, bangi, mirungi, skanka na dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuwakamata watuhumiwa 10,522.

“Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha mafanikio makubwa, kwani cha dawa za kulevya kilichokamatwa ni kiasi kikubwa kuliko kiasi kilichokamatwa wakati mwingine wowote nchini. Kiasi hiki ni karibu mara tatu ya kile kilichokamatwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ikiwa ni ishara ya dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupambana na janga hili” ,alisema Mhe. Jenista.

Alieleza kwamba hadi kufikia mwezi Disemba 2023, vituo vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics) vilivyohudumia waraibu 15,912 vilifikia 16, na nyumba za upataji nafuu (Sober Houses) na 56 zilizohudumia waraibu 3,488.

Waziri Jenista aliendelea kubainisha kwamba jumla ya waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipata huduma katika hospitali za wilaya, mikoa na rufaa nchini huku akisema Serikali imeanza ujenzi wa kituo cha Taifa cha Utengamao kwa ajili ya kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu.

‘Kituo hiki kitajengwa katika eneo la Itega Jijini Dodoma na kitasaidia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili waweze kujikimu kimaisha na kuepuka kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya,”alieleza.

Vilevile ameeleza kuwa, serikali imeweka jitihada kubwa katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa kuimarisha elimu na mikakati ya kukabiliana na tatizo hili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina, makongamano, mikutano, vilabu vya kupinga rushwa na dawa za kulevya shuleni na vyuoni.

Akibainisha mafanikio yaliyopatikana Waziri Jenista alieleza kwamba, mwaka 2023, Serikali ilianzisha kituo maalumu cha Habari na Mawasiliano (Call Centre) kilichopo katika ofisi za DCEA ambapo wananchi wanaweza kupiga simu namba 119 bila malipo na kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya au kupata elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya.

“Serikali imefungua Ofisi mpya tano za Mamlaka katika ngazi ya kanda ambazo ni nyanda za juu kusini ambayo ofisi zake ziko Mkoa wa Mbeya inahudumia Mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa Njombe na Iringa. Kaskazini ofisi zake ziko Mkoa wa Arusha inahudumia Mikoa ya Arusha, Manyara Kilimanjaro na Tanga,”alitaja Mhe. Jenista.

Akiendelea kutaja Miko hiyo alisema kuwa ni Pwani ambayo inatoa huduma  katika Mkoa wa Mtwara,Lindi, Ruvuma na Morogoro wakati  Kanda ya ziwa ambayo ofisi zake ziko Mkoani Mwanza inahudumia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu na Shinyanga, pamoja na Kanda ya kati yenye ofisi Mkoani Dodoma inayohudumia Mikoa ya Dodoma, Kigoma Singida na Tabora. 

Pamoja na mafanikio hayo alifafanua kwamba  bado Serikali imeendelea kuwekeza katika udhibiti  wa dawa za kulevya ambapo mwaka 2023 imenunua boti yenye kasi (Speed Boat) itakayotumika kufanya doria baharini kukabiliana na uingizaji wa dawa za kulevya kama vile heroine na methamphetamine.

Katika hatua nyingine Mhe. Jenista alisema Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024 ili kuhakikisha ushiriki wa wadau wote katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

“Sera hii itaimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zinazozalishwa nchini kama vile bangi na mirungi. Pia itatoa maelekezo ya kufanya utafiti wa mazao mbadala katika maeneo yanayolima mazao haya ili wananchi wapate kilimo cha mazao halali. Zaidi ya hayo, sera hii inaelekeza kuwajengea uwezo wadau mbalimbali katika udhibiti wa dawa za kulevya ili kuboresha ufanisi wa mapambano haya,” alisisitiza Mhe. Jenista.


Aidha Mhe. Jenista alitoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusisitiza kuwa elimu ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya inapaswa kuanzia ngazi ya familia pamoja na  Wazazi na walezi kushiriki katika kwa  kuwajengea misingi bora watoto wao ili wasijiingize kwenye vitendo viovu na makundi hatarishi yanayoweza kuwaingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post