Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAFUNZO YA LISHE KWA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII


Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utunzaji wa mazingira na utoaji wa msaada kwa watu wenye mahitaji maalum, Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS) kwa kushirikiana na Serikali kwa ufadhili wa Norwegian Church Aid (NCA) kwa fedha kutoka Norwegian Agency for Development Cooperation (Norad) limefanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wahudumu wa Afya ngazi ya jamii takribani 31 kutoka wilaya ya Kishapu na Shinyanga.

Mafunzo yamelenga kuwaelekeza njia bora ya kutatua changamoto ya udumavu na utapiamlo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa kufanya uchunguzi na kuwaanzishia lishe tiba watoto watakaobainika kuwa na hali ya udumavu kwa kutumia vyakula vinavyopatikana kwenye mazingira yanayowazunguka.


Akizungumzia mradi huo Afisa Miradi TCRS Kishapu bi. Mwanamina Jumanne Mavura amesema mafunzo hayo yametekelezwa kwa ushirikiano na maofisa lishe wa halmashauri za Wilaya ya Kishapu na Shinyanga.

Ameongeza kuwa, mradi wa Usalama wa Chakula na Kupunguza njaa (Food Security and Reduction of Hunger) unawezesha wakulima kuendeleza kilimo cha bustani kwa njia ya umwagiliaji kwa matone, ufugaji wa kuku walioboreshwa pamoja kuanzisha vikundi vya kijamii ambavyo vitaendeleza shughuli za huduma ndogo za fedha kwa njia ya kuweka na kukopa.


Shughuli zote hizi zinachangia kuongeza usalama wa chakula na hivyo kuboresha hali ya lishe.

Aidha ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuboresha hali ya lishe na kuondoa changamoto ya udumavu na utapiamlo katika jamii ambapo wahudumu wa Afya ngazi ya jamii takriban 31 wamepata mafunzo kwa siku mbili ambazo ni tarehe 24-25 Aprili 2024.


Afisa Lishe halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga bw. Saidi Mankiligo kutokana na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kishapu na Shinyanga kufanana ikolojia na ukame na hali duni ya Lishe na usalama wa chakula kuwa mdogo, Shirika la TCRS limeamua kushirikiana na Serikali kutekeleza mradi wa Usalama wa Chakula na Kupunguza njaa ambapo katika Wilaya ya Shinyanga mradi unatekelezwa katika Kata ya Mwalukwa ukijimuisha vijiji vine vya Bulambila, Ng'hama, Kadoto na Mwalukwa.


Kwa upande wake Afisa Lishe halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bi. Hadija Ahmed; ameainisha kuwa mafunzo yaliyotolewa kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ni chachu ya kutokomeza udumavu na Utapiamlo na kuongeza kuwa mafunzo yamelenga kwenye Lishe kwa Mama mjamzito na Lishe kwa watoto chini ya miaka mitano bi. Hadija ameongeza kuwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mradi unanufaisha wananchi kwenye vijiji vya Mwamasololo, Ididi, Bugoro, Mipa na Dulisi and Mwakolomwa (kata ya Sekebugoro); Wishiteleja na Kabila (kata ya Mondo).


Pia ameongeza kuwa wahudumu wa afya wamefundishwa kufanya uchunguzi wa lishe kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa kutumia kipimo cha MUAC – TAPE hali ambayo inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.

Nao baadhi ya wahudumu wa Afya ngazi ya jamii waliopatiwa mafunzo hayo wamelishukuru shirika la TCRS pamoja wafadhili ambao ni shirika la NCA kuja na mpango wa kuwajengea uwezo na kushauri mafunzo zaidi yaendelee ili kupata ujuzi zaidi wa kuibadilisha jamii na kuleta mabadiliko ya kiuchumi.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com