Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKUSANYA MAPATO KISHAPU WASHUKIWA,DED APEWA MAELEKEZO

Katibu Tawala msaidizi Mkoa wa Shinyanga , Ibrahimu Makana akizungumza kwenye kikao cha robo ya tatu cha balaza la madiwani Wilayani Kishapu mkaoni humo kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

Na Sumai Salum - Kishapu 

Katibu Tawala Msaidizi Mkoani Shinyanga, Ibrahimu Makana amewataka wakusanya mapato wa halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kuhakikisha wanafuata sheria, taratibu,kanuni na muongozo wa kazi zao katika kukusanya na kuhifadhi fedha za serikali.

Akizungumza leo Mei 9,2024 katika kikao cha robo ya tatu 2023/2024 cha Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu amesema mpaka kufikia Aprili 30 mwaka huu kiasi cha Tsh. Milioni 15.3 zilikuwa mikononi mwa wakusanya mapato jambo ambalo ni kinyume na taratibu na miongozo ya kazi.

"Wakusanya mapato mnakumbushwa tena mnapaswa kuweka fedha hizo ndani ya masaa 24 kwenye akaunti ya Halmashauri na sio kukaa mikononi mwenu pitieni tena ka makini kanuni na miongozo ya kazi zenu jambo hili lisijitokeze" amesema Makana

Aidha amemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anawawezesha vizuri watu hao na kupata muda wa kukaa nao kila baada ya wiki na kuzungumza nao atambue maendeleo yao ili wafikie lengo la ukusanyaji mapato waliojiwekea ikiwa ni 100%  ikiwa hivi sasa ni 64%.

"Kitu kingine Mkurugenzi hakikisha  watu hawa hawakai eneo moja kwa muda mrefu kwani itasababisha kupunguza uaminifu, na pia tunapoendelea ukusanyaji mapato kupitia mazao ya pamba,mpunga pamoja na zao la kunde inahitaji uadilifu na uaminifu mkubwa", ameongeza Makana.

Makana ameipongeza Halmashauri  ya Kishapu hasa madiwani kwa usimamizi mzuri wa hoja na kwa kushirikiana na watendaji kufanya kazi kwa weledi,umakini mkubwa jambo lililopelekea kupata hati safi ya ukaguzi wa nje kwa mwaka 2022/2023.

Kikao cha robo ya tatu cha balaza  la madiwani mwaka wa fedha 2023/2024 kimeambatana na uwasilishwaji taarifa za kamati mbalimbali ikiwemo Kamati ya uchumi ujenzi na mzingira,Kamati ya afya, kamati ya fedha na Kamati ya huduma za jamaii.
Kaimu Katibu tawala Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Fadhili Mvanga akizungumza kwenye kikao cha robo ya tatu cha baraza la madiwani ambapo amewashauri watendaji na madiwani kuibua vyanzo vipya vya mapato huku wakusanyaji wakizingatia uadilifu kwenye ukusanyaji mapato.
Mwenyekiti wa kamati wa huduma za jamii na Diwani wa Kata ya Kishapu Mhe. Joel Ndettoson akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha robo ya  tatu cha madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com